Wednesday, December 25, 2013

Slaa amsomesha JK

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amemshauri Rais Jakaya Kikwete kukomesha vitendo vya kikaburu vinavyofanywa na serikali yake, ikiwa anataka aishi kwa amani akistaafu.

Slaa akizungumza na waandishi wa habari wakati akihitimisha ziara yake katika majimbo 19 ya mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Singida, alisema hali ya nchi ni mbaya na ni wakati wa Rais Kikwete kuliepusha taifa na umwagaji wa damu kwa kusafisha alichokiita ‘uchafu’ serikalini.

Slaa alisema vyombo vya serikali vinaendesha matendo ya kikatili kwa wananchi wake, na kila sehemu alikopita kuna vilio vya mateso.

Alisema orodha ya manyanyaso wanayofanyiwa wananchi na polisi, wakuu wa wilaya, watendaji wa vijiji, kata na madiwani ni ndefu kiasi cha kuvuka hata yaliyofanywa na makaburu wa Afrika Kusini.

“Yapo mengine ya kubambikia kesi watu, kunyang’anywa ardhi, kunyimwa haki kwa nguvu tu, kuchangishwa michango haramu inayoambatana na vipigo na kunyang’anya watu mali zao, huku mapato na matumizi hayasomwi na nyingine kero kubwa kabisa ya migogoro ya ardhi.

“Watu wanateswa sana; wanaingizwa misumari na wanawekewa chupa sehemu za siri. Wananchi wanapigwa, kuteswa na kuuawa bila hata hatia. Tumefikia mahali serikali inawatenda raia wake ukatili mkubwa unaozidi hata ule wa makaburu wa Afrika Kusini. Tunakwenda wapi. Kikwete chukua hatua,” alisema.

Dk. Slaa alisema katika hali ya kushangaza viongozi wa serikali za vijiji vya Kakonko, Wilaya ya Buyungu na Kasulu Vijijini kutoka CHADEMA wamebambikwa kesi ya mauaji, huku wachimbaji wadogo wadogo huko Nzega wamepigwa vibaya na askari polisi na machimbo yao yametekwa na viongozi wa wilaya.

Amesisitiza kuwa kama Serikali ya Rais Kikwete inataka kupata uhalali mbele ya Watanzania na iwapo rais mwenyewe anataka kumaliza muda wake na kuacha kumbukumbu kwa wananchi, sharti sasa akomeshe mara moja mateso wanayofanyiwa wananchi.

No comments:

Post a Comment