Saturday, December 21, 2013

Dk. Slaa: Bunge lichunguzwe kwa ufisadi

SIKU chache baada ya wabunge kuumbuana kwa kuchukua fedha za safari bila kwenda wanakotakiwa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ametaka Ofisi ya Bunge ichunguzwe haraka.
Dk. Slaa ametoa kauli hiyo mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui, alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika maeneo ya Tura na Kigwe, jimboni Igalula katika ziara yake ya kuimarisha chama.
Alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), anapaswa kufanya ukaguzi maalumu haraka kwa Ofisi ya Bunge kutokana na harufu ya ufisadi kwenye matumizi ya taasisi hiyo.
Aliongeza kuwa amenasa nyaraka za siri, zikiwemo barua za Katibu wa Bunge kwenda hazina zikiomba mabilioni ya fedha ambayo matumizi yake yanafichwa kwenye kichaka cha safari za ndani na nje.
Aliongeza kuwa fedha hizo zinanuka uvundo wa ufisadi unaofanywa na taasisi hiyo kisha kuuhalalisha kwa vitu visivyolingana na thamani ya rasilimali iliyotumika wala havina tija kwa wananchi.
“Hatuna tatizo kabisa na wabunge kuchunguzwa au kukaguliwa… wakaguliwe wote kabisa… waliofanya safari za ndani na nje ya nchi, ninawajua wabunge… wapo wanaoghushi hata risiti ili wapate malipo. Wapo wabunge badala ya kuwa watetezi wa mali za umma wamegeuka kuwa mstari wa mbele kuhujumu wananchi wao,” alisema.
Aliongeza kuwa amenasa barua mbili za siri zilizoandikwa mwaka huu na Katibu wa Bunge kwenda hazina zikiomba jumla ya sh bilioni 52 ambazo zimetumika ndani ya miezi sita, huku matumizi yake yakiacha shaka kubwa.
“Barua ya kwanza inaomba jumla ya bilioni 23 kwa ajili ya matumizi ya Julai-Oktoba mwaka huu. Kwa wasiojua, fedha hizi zinaweza kujenga takribani madarasa 300 yaliyokamilika yenye kila kitu bila kumchangisha mwananchi wangu hapa hata senti moja.
“Bunge limeomba fedha hizi kwa ajili ya posho ya jimbo, kwa ajili ya gharama za mkutano wa 14, gharama zenyewe hazijaonyeshwa hapa, pia wameomba kwa ajili ya kamati za Bunge, nyingine ni kwa ajili ya Kamati Teule, Kamati ya Uchunguzi, pia wameomba bilioni 1 kwa ajili ya ziara za nje ya nchi za kamati.
“Kwa ajili ya ziara za kikazi ndani na nje ya nchi wameomba milioni 300 ambazo ni sawa na kituo kimoja cha afya kilichokamilika bila kuwachangisha wananchi.
“Bunge limeomba kwa ajili ya matibabu ndani na nje ya nchi jumla ya shilingi milioni 130, ambazo wangeweza kuzitumia kujenga hospitali nzuri hapa nchini kila mtu anaweza kutibiwa, kwa ajili ya uendeshaji ofisi na mikataba gani sijui wameomba bilioni 1,” alisema.
Katika barua ya pili, Dk. Slaa amedai kuwa Bunge limeomba sh bilioni 29 kwa ajili ya Oktoba hadi Desemba, huku akisema fedha hizo zingeweza kutumika vizuri kwa manufaa na maslahi ya Watanzania ambao bado wanahangaika kupata huduma za msingi ndani ya nchi yao.
“Hivi hizi fedha zingeweza kulipa madeni na mishahara ya walimu wangapi? Zingejenga barabara za vijijini ngapi? Zingehudumia wananchi kiasi gani katika elimu, afya au maji bila kuwachangisha michango ya ajabu ajabu? Hivi kuna mtu anaweza kuniambia thamani ya fedha za posho ya jimbo endapo hata wabunge hawaji majimboni kama huyu wa kwenu?” alisema Dk. Slaa.
Alibainisha kuwa chombo hicho muhimu kwa ajili ya kuwasemea na kuwawakilisha wananchi kimeanza kupoteza maana kwa wabunge wakisaidiwa na kiti, kuanza kujikita katika masuala yasiyokuwa na umuhimu wowote kwa Watanzania wanaotaka kuwasikia wakijadili maslahi ya watu waliowatuma bungeni.
“Bunge limeacha kazi ya kutetea, kusemea na kuwakilisha wananchi, badala yake, wanageuza Bunge sehemu ya majungu, vijembe, umbea wakisaidiwa na spika au naibu spika kulinda mambo hayo ya ajabu.
“CAG afanye huo ukaguzi maalumu, tunataka kujua thamani ya fedha za walipa kodi Watanzania hawa. Wanapanga ufisadi mkubwa kama huu kisha wanatafuta namna ya kuuhalalisha kwa kupanga safari zinazoitwa za kazi au mafunzo wakati hazina mpango wowote wala manufaa kwa Mtanzania,” alisema Dk. Slaa.

No comments:

Post a Comment