Monday, November 4, 2013

Muswada wa Katiba watinga Bungeni

Hatimaye Bunge limepokea Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa Mwaka 2013 kutoka serikalini, ambao unatarajiwa kuwasilishwa bungeni kwa hati ya dharura, katika Mkutano wake wa 13 unaoendelea leo.

Muswada huo, ambao tayari umekwishasainiwa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuanza kutumika kuwa sheria rasmi, utarudishwa bungeni ili kuwapa fursa wabunge ya kujadili mapendekezo ya kuuboresha.

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, na vyama vya siasa vyenye uwakilishi na visivyokuwa na uwakilishi bungeni, kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu.

Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alilithibitishia NIPASHE jana kuhusu muswada huo kupokelewa na Bunge.

“Tayari tumeshaupokea,” alisema kwa kifupi Ndugai alipojibu swali la NIPASHE lililotaka kujua kama Bunge limeshaupokea muswada huo au la.
Hata hivyo, alisema muswada huo unasubiri kupelekwa kwenye Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa ajili ya maamuzi.

Serikali iliahidi kuupeleka bungeni muswada huo kwa ajili ya kujadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa sasa.

Pamoja na kwamba muswada huo haujaorodheshwa kwenye ratiba ya shughuli za Mkutano wa sasa wa Bunge, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Habari za Bunge, Deogratias Egidio, alisema Bunge linaweza kufanya shughuli yoyote, ambayo haipo kwenye orodha hiyo ya awali ikiwa itakidhi matakwa ya kikanuni kama litaona inafaa.

Hivyo, matarajio ya kurudishwa bungeni ni makubwa, hasa kwa vile unatarajiwa kurudishwa kwa hati ya dharura.

Iwapo muswada huo utarudishwa bungeni, basi mjadala wake unatarajiwa kutawala zaidi Bunge na kuwagawa wabunge kwa mara nyingine.

Utabiri huo unaweza kutimia kwa kuwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, walisusia na kutoka nje wakati wa kujadili na kupitishwa kwa muswada huo wakidai kwamba una kasoro kadhaa.

Kasoro hizo ni kutoshirikishwa kwa Zanzibar katika kuupitia na kuuchambua, madaraka ya Rais ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuvunjwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba baada ya kuwasilisha Rasimu badala ya kuendelea kuwapo hadi kura ya maoni.


Vyama hivyo licha ya wabunge wake kususia Bunge, pia viliunda ushirikiano wa kupinga mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa maelezo kuwa umehodhiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hatua nyingine, Mkutano wa 13 wa Bunge ulioanza Oktoba 29, mwaka huu, unaendelea leo, kwa kuanza na kipindi cha maswali ya kawaida.

Baada ya kipindi cha maswali, serikali itapata fursa kujibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/2015, wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Mkutano huo, kesho baada ya kipindi cha maswali ya kawaida, utawasilishwa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013.

Muswada huo utajadiliwa na wabunge kwa siku mbili mfululizo, kuanzia kesho hadi keshokutwa (Jumatano).

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa, Alhamisi, kutakuwa na kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu na baadaye yale ya kawaida.

Baadaye, utawasilishwa Muswada wa Kura ya Maoni wa Mwaka 2013, ambao wabunge wataujadili kwa siku tatu mfululizo, kuanzia siku hiyo hadi Jumamosi wiki hii kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa hoja ya kuahirisha Bunge. 

No comments:

Post a Comment