Sunday, November 3, 2013

Mnyika amshukia Rais Kikwete

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema migogoro iliyojitokeza wakati wa Operesheni Tokomeza Majangili haiwezi kutenganishwa na agizo la Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifungua mafunzo ya wajumbe na viongozi wa CHADEMA kutoka kata 35 kati ya 37 zinazounda Jimbo la Dodoma.
Alisema pamoja na baadhi ya wabunge wa CCM kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi kuwajibika, Rais Kikwete hawezi kuachwa kando.
Alisisitiza kuwa Rais Kikwete asiwekwe kando kwani sababu kubwa ya mifugo ya wafugaji na wao wenyewe kuuawa, kumetokana na udhaifu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayoongozwa na Rais Kikwete.
Mnyika alimtaka Rais Kikwete kutonyamaza bali atoe tamko kwanini Operesheni Tokomeza Ujangili imegeuka kuwa tokomeza mifugo na mauaji ya wafugaji.
“Pamoja na ukweli kuwa baadhi ya mawaziri wana udhahifu katika kusimamia operesheni hiyo, lakini Rais Kikwete naye anapaswa kujiuliza na kuwajibika kwanini yametokea hayo na yeye amekaa kimya hadi Bunge limefikia hatua ya kujadili jambo hili kwa uzito mkubwa?
“Haiwezekani Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa CCM na kiongozi wa nchi akanyamaza bila kutoa tamko, kwanini matukio hayo yametokea badala ya kupambana na majangili askari wanapambana na wafugaji na mifugo yao,” alisema.
Akiendelea kuzungumza na viongozi hao wa kata, Mnyika alisema CCM pamoja na serikali yake haina nia njema na wafugaji kwani kila kinachotendeka kina baraka ya serikali ya Rais Kikwete.
Aidha, alisema kuna kila sababu ya viongozi wa CHADEMA kuhakikisha wanasimamia vema mchakato wa rasimu ya Katiba mpya kwa kuhakikisha wanapiga kelele ili Katiba mpya iwe na kipengele cha kumruhusu Mtanzania kumiliki rasilimali ardhi.
Alisema haiwezekani Mtanzania asiwe na uhakika wa kumiliki ardhi, kwani kwa Katiba ya sasa ambayo ni mbovu inampa madaraka makubwa na ardhi yote ni mali ya rais.

No comments:

Post a Comment