CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa hivi karibuni nchini Uingereza katika mkutano wa Open Government Partneship (OGP) kuwa serikali yake inasimamia uwazi na uwajibikaji ni ya kujikosha mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, ilieleza Serikali ya Rais Kikwete inaendeleza usiri na udhaifu wa kiutendaji kwa kuvifungia vyombo vya habari kwa madai ya kuandika siri za serikali.
Mnyika alisema kauli hiyo ya Rais Kikwete ni ya kujichanganya na watendaji walio chini yake kwa kile alichoeleza tayari Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni ilishaweka wazi kuwa muswada wa uhuru wa vyombo vya habari utafikishwa bungeni baada ya mchakato wa katiba mpya kukamilika.
“Rais anasema muswada wa uhuru wa taarifa utawasilishwa bungeni Aprili 2014, majibu yake mbele ya mkutano huo yalikuwa ni ya kujikosha zaidi kwa kuwa ni serikali yake ndiyo inaendeleza usiri na ubabe dhidi ya uhuru wa habari kama ambavyo imefanya kwa kuyafungia baadhi ya magazeti hapa nchini,” alisema Mnyika.
Alisema rais kama ana nia ya dhati ya serikali yake kuwasilisha muswada huo kabla ya katiba mpya kupatikana, ajitokeze hadharani na azungumze na taifa kuonyesha kuondoa usiri kwa kuagiza sheria ya siri za serikali iandikwe upya.
Aliongeza kuwa ni wakati muafaka kwa muswada wa uhuru wa taarifa ulioandaliwa na wadau mwaka 2007 kisha kukabidhiwa serikalini usomwe kwa mara ya kwanza katika Bunge hili.
Mnyika alisema kama Rais Kikwete hatotoa majibu baada ya kurejea nchini, atawasilisha muswada huo bungeni kwa niaba ya wadau mbalimbali kwa lengo la kuufanya mchakato huo uende kwa haraka.
No comments:
Post a Comment