MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaachia huru Waziri wa zamani, Arcado Ntagazwa na wenzake waliokuwa na kesi na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu zenye thamani ya sh milioni 74.9, baada ya kuwaona hawana hatia na hawakutenda kosa hilo.
Sambamba na hilo, mahakama hiyo imemshauri mlalamikaji katika kesi hiyo ambaye ni Noel Severe kufungua kesi ya madai kama walivyofanya hivi karibuni, ambapo walifungua kesi ya madai dhidi ya Ntagazwa.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Gene Dudu, alisema kuwa kesi hiyo ya jinai namba 108/2012 aliyoitolea hukumu jana, haikupaswa kuwa jinai bali ya madai.
Akisoma hukumu hiyo, saa tano asubuhi, Dudu alisema upande wa Jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Charles Anindo, katika harakati zake za kutaka kuthibitisha kesi yake ulileta mashahidi watano wakati upande wa washitakiwa waliokuwa wanatetewa na wakili wa kujtegemea, Alex Mshumbusi, ulileta mashahidi wanne, ambao ni washitakiwa wenyewe na shahidi mmoja.
Hakimu Dudu alisema mahakama yake ilipata fursa ya kuchambua ushahidi wa pande zote mbili na mwisho wa siku ikabakiwa na swali moja la kujiuliza kuwa, je, ni kweli washitakiwa hao walitenda kosa kinyume cha kifungu cha 320 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002?
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa kifungu hicho ni lazima mtuhumiwa awe ametoa taarifa za uongo kwa mlalamikaji ili ajipatie kitu fulani kwa njia hiyo ya uongo na awe na nia ovu wakati akitaka kujipatia mali hizo.
“Lakini kwa mujibu wa ushahidi uliopo mahakamani, imeonesha wazi kabisa Ntagazwa na mshitakiwa wa pili ambao ni wajumbe wa bodi wa taasisi ya Ford walitoa oda kwa Kampuni ya Visual Storm ambayo Mkurugenzi wake ni Severe, ya kuomba watengenezewe fulana 5,000 na kapelo Korea 5,000, ambapo walifanya hivyo baada ya kikao cha bodi kutenga bajeti ya kutengenezwa kwa mavazi hayo.
“Mavazi hayo yaligawiwa bure kwa umma siku ya kumbukumbu ya kifo cha hayati Julius Nyerere, wakiwa na lengo la kutokomeza ufisadi wakati wa kumuenzi kiongozi huyo, kwa ahadi kuwa wangelipa ndani ya mwezi mmoja,” alisema Dudu.
Alisema hoja ya kwamba mshitakiwa wa tatu ambaye ni mtoto wa Ntagazwa, Dk. Webhale Ntagazwa, kuwa ndiye alitoa oda ya kuchapwa kwa fulana na kofia hizo, hakustahili kushitakiwa kwa kosa hilo kwa sababu Ford ni taasisi na si mali ya mshitakiwa.
Dudu alisema utetezi wa washitakiwa unaonesha waliandika barua kwa wafadhili wakiomba fedha za kuweza kufanikisha mradi wao wa kutaka kumuenzi Nyerere siku ya kumbukumbu ya kifo chake Oktoba 14, na wafadhili hao waliwakubalia waendelee na taratibu za kuchapisha fulana na kwamba watatoa fedha za kulipia.
Lakini kabla ya tamasha kufanyika, Ntagazwa na wenzake walishtukia fulana zao hizo zikibadilishwa nembo na kuonekana ni za Chama Cha Jamii (CCJ), hali iliyosababisha mfadhili aliyewaahidi fedha kujitoa akidai hawafadhili vyama.
“Mahakama hii imeona habari hiyo iliyochapishwa kwenye gazeti la Mtanzania, ambapo hata washitakiwa waliandika barua kwa IGP Said Mwema kulalamika fulana na kofia zao kuhujumiwa, hivyo kusababisha washitakiwa wajikute wakishindwa kulipia gharama za uchapishaji kwa kampuni ya Severe baada ya mfadhili wao kujitoa,” alisema.
Baada ya hakimu huyo kusoma hukumu, Ntagazwa aliangua kilio nje ya mahakama akisema: “Yaani kumuenzi Nyerere ndiko kulikosababisha nifunguliwe kosa la jinai? Tena polisi walivyo na roho mbaya na katiri siku wanakuja kunikamata nyumbani walinikamata uchi wa mnyama nikiwa bafuni naoga kwa sababu nimehamia CHADEMA.”
Mbali na Ntagazwa, washitakiwa wengine ni mtoto wake, Dk. Webhale Ntagazwa na mshitakiwa wa kwanza ni Senetor Mirelya (60).
Aprili 23, mwaka 2012, ilidaiwa mahakamani hapo na wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya, kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani Mikoroshini, washitakiwa hao kwa nia ovu walijipatia fulana 5,000 na kofia 5,000 zenye thamani ya sh milioni 74.9 kutoka kwa Noel Severe, kwa makubaliano kuwa wangemlipa katika kipindi cha mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini walishindwa.
No comments:
Post a Comment