Tuesday, October 29, 2013

Njelu Kasaka afichua siri ya Nyerere

ADAI ALITAMANI SERIKALI TATU, AWASHANGAA CCM KUKWEPA
KADA mkongwe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ni muasisi wa kundi la wabunge waliokuwa wakishinikiza hoja ya Serikali ya Tanganyika, maarufu kama G55, Njelu Kasaka, ameibuka na kuwashangaa wabunge wa chama hicho kupinga hoja ya muundo wa serikali tatu wakati ni yao tangu awali ya kudai mabadiliko ya muundo wa Muungano.
Kasaka aliongeza kuwa hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliona umuhimu wa muundo huo wa serikali tatu, isipokuwa alitoa tahadhari kuwa kwa aina ya uendeshaji wa serikali uliokuwa unaendekezwa kwa kuogopana na kulindana Muungano usinge dumu.
Mwanasiasa huyo ambaye amewahi kuwa mbunge wa Lupa, alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na gazeti hili jijini Dar es Salaam, huku akiwaasa wabunge hasa wa CCM kuacha mzaha katika suala la katiba, akisema ni muhimu na lisipoangaliwa kwa umakini linaweza kuliingiza taifa katika machafuko.
“Wabunge wote watakapokuwa Dodoma wajue wana dhamana kubwa sana, wasifanye mzaha na suala la katiba, ni suala muhimu kwani katiba mbaya inaweza kuangamiza. Suala la kubadilishwa katiba halifanyiki kama wanavyobadili sheria.”
“Wanapitisha leo, rais anasaini anawarudishia wakafanye mabadiliko, si kitu rahisi. Wakumbuke kuwa wakiamua vibaya wataangamiza taifa kwa muda mrefu na wakiamua vizuri watalisaidia taifa,” alisema.
Kasaka alitumia muda mwingi kuelezea historia ya kundi hilo (G55), akisema lilianzishwa baada ya manung’uniko ya Wazanzibari kuwa wanaonewa na Serikali ya Muungano.
“Wazanzibari walisema kuwa Serikali ya Tanganyika imejifanya kuwa ni ya muungano ili kuitawala Zanzibar bila ridhaa ya Wazanzibari na kwamba ilizuia Serikali ya Zanzibar kufanya mambo yake.
“Serikai tatu ni wazo la CCM, kwani wakati tunalianzisha vyama vya upinzani vilikuwa vingine havijasajiliwa na vilivyokuwapo havikuwa na wabunge, vilikuwa makundi ya wanaharakati wakati huo, waliunga mkono kutaka mabadiliko,” aliasa.
Kasaka aliongeza kuwa hali ya wakati huo ilimuudhi kwani mtu wa Bara alikuwa akitaka kwenda Zanzibar inabidi awe na hati ya kusafiria na kuchukuliwa kama mgeni wakati wanazungumzia nchi moja.
“Nilipeleka hoja bungeni, ikaungwa mkono na Matheo Qares, Arcado Ntagazwa, Mussa Nkhangaa, William Mpiluka (marehemu), Sebastian Kinyondo (marehemu) na Jenerali Ulimwengu. Kwa ujumla niliungwa mkono na wabunge 55, ingawa baadaye wabunge karibu wote walituunga mkono tukaambiwa halimo katika sera za CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, serikali tatu au mabadiliko ya muundo wa Muungano kutoka wakati huo hadi sasa hayaepukiki.
Kwamba, mtazamo wa Wazanzibari wanasema wapo tayari kutofautiana katika mambo yote kisiasa au kiitikadi lakini hoja ya Uzanzibari (identity ya nchi) haifi hadi utakapomwondoa Mzanzibari wa mwisho.
“Kumbuka kuwa aina ya Watanzania wa sasa si wale wa miaka 30 iliyopita, wakati huo walikuwa wanazaliwa, ila sasa wao ndio wasomi na wasemaji katika mambo mengi.
“Nawatahadharisha wabunge waangalie idadi ya Watanzania sasa si ile iliyokuwapo, mwamko wa sasa si ule wa miaka iliyopita. Mwaka 1993 -1995 watu waliokuwa wanajitambulisha ni wapinzani walikuwa wanazomewa, sasa wale wanaojitambulisha CCM ndio wanaozomewa, wakubali mabadiliko, serikali tatu haziepukiki na hii ilikuwa hoja ya wabunge wa CCM,” alisema.
Kisaka alisema wabunge wakubali kufanya marekebisho ya sheria iliyorejeshwa na rais, kwani serikali haiwezi kujitungia katiba, hivyo wabunge wote hasa wa CCM wakubali suala la serikali tatu, wafanye marekebisho mazuri ili kuondoa uwezekano wa mgogoro mkubwa kati ya Bara na Zanzibar.
Alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa mjini Dodoma hivi karibuni ya kukemea vitendo vya rushwa ndani ya chama, akisema itawaathiri kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ikiwa hawatajirekebisha.
Alisema anakubaliana na Kikwete kwa asilimia mia moja kwamba CCM isipoacha rushwa itaanguka, na isipoacha upendeleo na kulazimisha wagombea wasiokubalika vilevile itakufa.
Kasaka alimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua, asiishie kusema. Kwamba, anaweza kutumia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa masuala ya kisheria na mengine ya kiutendaji yapo chini ya uwezo wake.
“CCM watu hawachukuliani hatua, Makamu Mwenyekiti (Bara), Philip Mangula, alilalamikia rushwa aliposhindwa uenyekiti wa Mkoa wa Iringa, lakini aliishia kusema kuwa uongozi katika chama unapatikana kama bidhaa gulioni, na alipochaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wala hajawahi kuchukua hatua,” alisema.
Kasaka aliongeza kuwa hadi Rais Kikwete ameamua kujitoa kuyasemea hayo nje, ni kwa sababu ndani ya CCM watu si wasikivu, wengine wana dharau.
“Ukiona mke na mume wanatukanana hadharani ujue ndani wametukanana vya kutosha na imeshindikana, wameonyana imeshindikana, ndiyo maana wanakuja hadharani kuja kukemeana mbele yetu,” alisema.

No comments:

Post a Comment