Wednesday, October 30, 2013

Mwigamba `apigwa ngumi`nyingine

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemjibu aliyekuwa Mwenyekiti wake wa mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuwa Katiba ya chama hicho haijachakachuliwa kama anavyodai.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisa  Mwandamizi wa Habari wa chama hicho,  Tumaini Makene, madai ya Mwigamba yamejaa uongo, upotoshaji, uzushi na yenye lengo la kukichafua na kuchonganisha chama kwa kuwa ukweli halisi anaujua.

Alisema Chadema inashangazwa na hatua ya Mwigamba kuendelea kuvunja katiba, kanuni, maadili, miongozo, taratibu na itifaki ya chama, kwani kupitia vyombo vya habari ameendelea kutunga mambo yasiyokuwapo badala ya kuwasilisha hoja zake (kama anazo) kupitia vikao halali vya chama ambavyo yeye anao uwezo wa kuitisha au kuhudhuria. Aidha, taarifa hiyo iliambatana na ujumbe wa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, ambaye alikuwa Katibu wa Kamati iliyohusika na uandikaji upya wa Katiba ya Chama ya mwaka 2006, ambayo ndiyo inayotumika hadi sasa.

Alisema wakati wa mabadiliko ya Katiba mwaka 2006, kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano hakikuguswa.

Alisema madai ya Mwigamba ni kuwa wakati Katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela, jambo ambalo siyo kweli.
“Mwaka  2006 hatukufanya marekebisho ya Katiba bali tuliandika upya Katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004… waraka uliandikwa nchi nzima kwa wanachama kutoa maoni na kuwasilisha makao makuu kuanzia kwenye ngazi zao za chini za kikatiba,” alifafanua Mnyika.

Alisema baada ya kukusanya maoni kulikuwa na timu tatu, moja ilihusu kuandika falsafa na itikadi ya chama ambayo Mwenyekiti wake alikuwa Profesa Baregu na Katibu wake nilikuwa mimi (Mnyika).

“Sehemu hiyo ya Katiba niliandika neno kwa neno mapendekezo ya awali kwa kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa, tulifanya mapitio pamoja na Profesa Baregu na hatimaye ikaingia kwenye vikao vya kikatiba vya chama na kupitishwa,” alibainisha.

Alisema sehemu ya falsafa kwa sehemu kubwa ilinukuliwa kutoka kwenye Katiba kama ilivyokuwa mwaka 2004, sehemu ya itikadi iliandikwa upya kabisa haikuwapo katika Katiba ya Chadema ya zamani.

Mnyika alibainisha kuwa sehemu zingine yaliunganishwa maoni mapya na kufanya rejea kwenye Katiba ya zamani ilifanywa na timu ya watu watatu tukiongozwa na muasisi wa chama, Mzee Victor Kimesera, na Mkurugenzi Benson Kigaila na yeye (Mnyika).

Alifafanua kuwa kulikuwa na timu nyingine ya kuandaa miongozo ya mabaraza ya chama ambayo ni Baraza la Wazee, Bavicha na Bawacha ambao nao walifanya kazi kwa upande wao na nilishiriki katika kupendekeza mwelekeo na mapitio ya kulinganisha rasimu ya miongozo yao na rasimu ya Katiba ya chama.

“Kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano, hakijawahi kuingizwa kwenye Katiba mpya ya Chadema,” alisema Mnyika.

Alisema baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya Katiba ilipita katika vikao vyote vya kikatiba yaani sekretariati, Kamati Kuu, Baraza Kuu na hatimaye mkutano mkuu na kama kingekuwa kimetolewa Mwigamba angehoji tangu Agosti, mwaka 2006.

Alisema kumekuwapo pia mchakato wa kufanya marejeo kwa ajili ya kushughulikia makosa ya uchapaji kwa nyakati mbalimbali, suala hilo siyo kati ya mambo yaliyoibuliwa.

Alisema mwaka 2009, Chadema kilifanya uchaguzi mkuu wake mkuu nchi nzima na vifungu vya masuala ya uchaguzi wa ndani ya chama vilifanyiwa rejea mara kwa mara.
“Mwigamba alikuwapo wakati huo, suala hili la kwamba kuna kifungu kimeondolewa kinyemela sikulisikia likilalamikiwa kwenye vikao vyovyote vya kikatiba iwe ni sekretariati, Kamati Kuu, Baraza Kuu na mkutano mkuu,” alibainisha.

Alisema kwa vyovyote vile kwa historia ya chama kutoka mwaka kilipoanzishwa mpaka wakati huo wa uchaguzi wapo viongozi ambao walikuwa wanagombea wakiwa na vipindi viwili wakati huo kwenye cheo kimoja cha ngazi moja; kifungu hicho kingekuwapo kutoka 2006 kingetumika kuwawekea pingamizi na madai hayo hayajawahi kutolewa kokote kwenye vikao vya kichama.

Alisema madai kama hayo yakitolewa na kiongozi wa chama mwenye nafasi ya juu ukweli wote huo unaacha maswali kuhusu dhamira yake.

MWIGAMBA APEWA BARUA RASMI 
Wakati huo huo, Baraza la Uongozi la Chadema Mkoa wa Arusha, limeridhia uamuzi wa kumsimamisha uenyekiti wa mkoa, Samson Mwigamba, uliofanywa na Baraza la Uongozi la Kanda ya Kaskazini na limemwandikia barua rasmi ya kukoma kuwa kiongozi.

Pamoja na barua hiyo, uchunguzi dhidi yake unaendelea na iwapo Baraza la Uongozi la Mkoa litajiridhisha au kubaini mambo mengine zaidi dhidi yake linaweza kuchukua uamuzi wa kumwachisha uanachama.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema jana wakati akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kwamba barua ya kukoma uongozi tayari ilikuwa imekwisha kuandikwa na alitakiwa akabidhiwe juzi.

Hata hivyo, alisema Mwigamba hakupatikana juzi, hivyo waliamua jana wamtume kijana ili amtafute na kumfikishia barua hiyo.

Alisema pamoja na barua kwa Mwigamba, wametuma pia barua kwa Kamati Kuu makao makuu jijini Dar es Salaam kwa hatua zaidi za kufuata.

“Mwigamba alikiri kwenye kikao cha Baraza la Kanda kukiuka maadili, kwa hiyo pale pale anakoma kuwa kiongozi…hatua iliyofuata dhidi yake ni kwa Baraza la Uongozi la Mkoa kumwandikia barua ya kukoma uongozi, jambo ambalo tumefanya na dondoo za vikao kufikia hatua hiyo tumewasilisha makao makuu,” alisema.

Jumamosi iliyopita, Baraza la Uongozi la Kanda, lilitangaza kumsimamisha Mwigamba uongozi kwa muda usiojulikana wakimtuhumu kwa usaliti, uzushi, uzandiki na uchonganishi kwa viongozi.

Pamoja na kusimamishwa, uongozi wa chama wa Kanda ya Kaskazini ulimfikisha Mwigamba polisi kwa kutumia mtandao wa kijamii kukichafua chama hicho na viongozi wake.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Israel Natse, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alisema wakati Mwigamba amesimamishwa, chama kitaendelea na uchunguzi dhidi yake.

Alisema Mwigamba alisimamishwa Ijumaa jioni na kikao cha Baraza la Uongozi Kanda ya Kaskazini akituhumiwa kutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Jamii Forum taarifa za kuwatuhumu viongozi wa juu wa chama kuwa wamechakachua katiba.

Katika taarifa hiyo inayopatikana kwenye mtandao huo inasema ‘Kwa nini mabadiliko ya Chadema ni lazima’ imekuwa ikitoa taarifa za uzushi na uchonganishi.
Juzi Mwigamba alisema kuwa ameamua kukaa pembeni kusubiri uchunguzi wa chama dhidi yake.

NIPASHE

No comments:

Post a Comment