MBUNGE wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (CHADEMA), ameitaka serikali itoe maelezo ni kwanini inatumia fedha nyingi kununua samani zisizo imara.
Mtinda alitoa hoja hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza na kuitaka serikali ieleze ni lini itaacha mtindo huo.
“Serikali inatumia fedha nyingi kununua samani ambazo si imara na zinaharibika mapema, ni kwanini msiingie mkataba wa kununua samani hizo ambazo ni imara kupitia Jeshi la Magereza ili kuokoa fedha za mlipakodi?” alihoji Mtinda.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alitaka kuelewa kama wapo wafungwa wenye ujuzi mbalimbali hususani ufundi seremala na wanatumiwaje.
Pia alitaka kujua kama serikali inatumia ujuzi wa wafungwa hao hususani wale wa muda mrefu na kifungo cha maisha.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima, alisema serikali inatambua kuwa zinanunuliwa samani ambazo si imara.
Alisema kwa kutambua hilo tayari serikali imeanza kununua samani imara na za kudumu katika ofisi za wabunge mikoani.
Alisema Jeshi la Magereza lina utaratibu wa kuwatumia wafungwa wenye ujuzi katika kufanya kazi za uzalishaji mali kama vile ujenzi, kilimo na utengenezaji samani.
No comments:
Post a Comment