Wednesday, October 30, 2013

Mbowe ahoji uonevu operesheni kimbunga

MBUNGE wa Hai, Freeman Mbowe (CHADEMA), ameikalia kooni serikali na kuihoji kama itakuwa tayari kuwalipa fidia watu ambao watagundulika kuonewa katika Operesheni Kimbunga inayoendelea hivi sasa.
Alisema pamoja na nia njema ya serikali ya kuwaondoa  wahamiaji haramu lakini zoezi hilo limefanyika katika mazingira ambayo hayakuwa na maandalizi ya kutosha.
Mbowe alisema kutokana na sababu hizo yapo maeneo ambayo yalionekana kabisa chuki na uonevu umetumika kwani kuna watu ambao wameondolewa kinyume na haki za binadamu na wengine bila kujali mali zao ama mazingira waliopo wakiwa ndani ya Tanzania.
“Je, kwa sababu na uonevu mkubwa uliojitokeza au kuendana na zoezi hili pale itakapogundulika kwamba vyombo vyetu vilitumia utaratibu ambao ni kinyume cha sheria na uvunjaji wa haki za binadamu, serikali itatakiwa kulipa fidia kwa watu watakaobainika kuwa wameonewa katika zoezi hili?” alihoji.
Akitolea ufafanuzi suala hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, alikiri kuwepo kwa malalamiko kuhusiana na baadhi ya watu kuondolewa kinyume cha haki za binadamu.
Kuhusu serikali kuwalipa fidia, alisema serikali itafanya linalowezekana kulichunguza jambo hilo na iwapo ikibainika itachukua hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria za nchi ya Tanzania.
Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Bumbwini, Ramadhan Haji Saleh (CCM), alitaka kujua serikali inachukua hatua gani za ziada kuwatoa wahamiaji haramu nchini ambao wamekimbilia mikoa mingine nchini.
Akijibu swali hilo, Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, alisema ili kuweza kufanikisha zoezi hilo wameamua kufanya operesheni za kushtukiza katika mikoa mbalimbali yenye lengo la kuwabaini wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua.

No comments:

Post a Comment