CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema Watanzania hawana sababu ya kutafuta ushahidi mwingine wa kuiondoa madarakani Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zaidi ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwa rushwa iliyokithiri itakiondoa chama hicho.
Marando ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Pwani na mjumbe wa Kamati Kuu, alitoa kauli hiyo jana wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika majimbo ya Kibiti na Rufiji ikiwa ni kuimarisha chama katika kanda hiyo.
Alisema Rais Kikwete baada ya kutafakari kwa kina hatma ya Tanzania, amebaini nchi kuendelea kuongozwa na CCM ni kuendelea kuiangamiza na kuamua kutumia ushauri wa busara kwa wananchi waachane nayo.
“Mnasubiri kauli gani nyingine kwa ajili ya kuiweka CCM pembeni ikiwa mwenyekiti wake ameshaona hatari ya chama chake kuendelea kuongoza kutokana na kukithiri kwa rushwa?” alihoji.
Marando alisema njia nzuri ya wananchi kuenzi kauli ya Rais Kikwete, ni kuikataa CCM katika kila uchaguzi utakaojitokeza ndani ya nchi.
Akizungumzia tofauti ya CHADEMA na CCM, alisema inaonekana wazi katika mahitaji ya kusimamia elimu na afya.
Alisema ili nchi iendelee, inahitaji watu wake wawe na elimu bora jambo aliloeleza kuwa Serikali ya CCM haitaki kuwafikisha huko ili waendelee kuwatawala.
“Tusipopambana hapa watoto wetu wataendelea kuwa wapiga kura na watoto wao wataendelea kuwa wapigiwa kura kila siku, kwa maana itafika wakati vigezo vya kuwania nafasi za kisiasa zitahitaji elimu ambayo hatukupatiwa kwa makusudi,” alisema.
Kuhusu afya, alieleza kuwa ni wakati wa serikali kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya pasipo kujali hali zao za kiuchumi, na kwamba hospitali zote za serikali zinastahili kutoa huduma bora kama inavyopendekezwa na CHADEMA.
Alisema ni aibu rais wa nchi kusimama hadharani na kusema Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza katika utafiti wa gesi kwa kuwa jukumu la kuwawezesha linapaswa kusimamiwa na serikali ya nchi husika.
Marando alisema serikali imeshasaini mikataba mingi ya gesi pasipo kuwepo sera rasmi ya rasilimali hiyo jambo aliloeleza kuwa ni ubabaishaji wa makusudi.
Naye Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa CHADEMA, Mwita Mwikabwe, alisema maisha ya wakazi wa Pwani juu ya maendeleo yao yanaamuliwa kwa kunyoosha vidole badala ya kujengewa hoja.
Alisema mkoa huo wabunge wake wote wanatokana na CCM huku kukiwa na madiwani wachache wa vyama vya upinzani, jambo aliloeleza kuwa linawarudisha nyuma kimaendeleo.
“Leo wapinzani wakijenga hoja juu ya mustakabali wa maisha yenu, wabunge wenu hawatoi hoja badala yake wanasema tunyooshe vidole kujua kama kuna shida kwa Watanzania, na kwa kuwa wapo wengi, wanashinda huku ninyi mkiendelea kuwa katika hali mbaya kimaisha,” alisema.
No comments:
Post a Comment