CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilaya ya Ilala, kimelishutumu Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutokana na vitendo vyake vya kuzuia mikutano ya chama hicho kinyume cha sheria.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa chama hicho Wilaya ya Ilala, Matius Ijumba, alisema jeshi hilo limekuwa likivinyanyapaa vyama vya siaasa katika suala zima la kufanya mikutano.
Alisema jeshi hilo hivi karibuni limezuia mkutano wa hadhara wa chama hicho uliokuwa ufanyike Oktoba 26 mwaka huu kwa madai kilikuwa hakina kibali kutoka Serikali ya Mtaa wa Kivukoni.
Ijumba alisema kauli hiyo haina ukweli kwani chama hicho Oktoba 21 mwaka huu kililiandikia jeshi hilo barua yenye kumbukumbu DSM/Ilala/so7/2/vol.11/179 ya kuomba kibali.
“Tunauliza ni sheria ipi inayowapa nguvu polisi kuombwa kibali kwani polisi katika hili wanapaswa kupewa taarifa kwa ajili ya kuimarisha usalama kwenye mikutano hiyo!” alisema Ijumba.
Alisema barua ya kuomba kibali ilipelekwa mapema lakini cha kushangaza hawakujibu hadi Oktoba 26 mwaka huu saa 7:00 mchana ndipo ilijibiwa kuwa chama hicho hakikupeleka barua ya serikali ya mtaa.
“Hapa kuna mchezo unaofanyika kwani hii ni mara ya pili mkutano wetu unazuiwa kwa mazingira kama haya ya kutupiana mpira kati ya polisi na watendaji wa serikali ya mtaa. Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 19,” alisema Ijumba.
No comments:
Post a Comment