Monday, October 7, 2013

Lissu: Tutamjua Rais Kikwete leo

ASEMA KAULI ZAKE WANATAKA WAZIONE KWENYE KAMATI YA KATIBA
MNADHIMU wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu, amesema kuwa watapima kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu muswada wa sheria ya mabadiliko ya katiba, watakapokutana leo katika Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Lissu alisema kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa juzi alisema kuwa suala hilo linazungumzika.
“Mimi ninataka kuona leo kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala liwepo suala hilo katika ratiba kati ya mambo yatakayojadiliwa tayari kwa ajili ya kurejesha muswada bungeni.
“Kama suala hilo halitakuwepo, basi hotuba ya rais itakuwa ni porojo za Magogoni (Ikulu). Rais asiposaini muswada huo ataonyesha nia nzuri aliyokuwa nayo, na hayo tuyaone katika ratiba ya kamati,” alisema.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na msemaji mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Katiba na Sheria, alieleza mshangao wake kwa Rais Kikwete kuhutubia taifa kwa habari za kuambiwa, kuelezwa na kufahamishwa bila yeye kujiridhisha.
Alisema kuwa rais alimtuhumu kwa kumuita “mzushi na muongo mtupu mwenye kauli za kinafiki, fitina na uzandiki wa hali ya juu”, lakini akahoji ni kwanini anawataka wapinzani wakae mezani wazungumze naye wakati ni waongo.
“Hoja zangu zilihusu Zanzibar kutokushirikishwa katika mchakato wa kuboresha muswada wa mabadiliko ya sheria, nilisema hakuna mdau hata mmoja au mtu binafsi aliyeonana na wajumbe wa kamati.
“Kwa upande wa bara kulikuwa na wadau 22, ukijumlisha na vyama vya siasa 22, hivyo bara peke yake tulisikiliza wadau 44. Je, fitina, uzandiki na uongo anauosema Kikwete upo wapi?” alihoji.
Lissu alitaja baadhi ya taasisi za bara walizokutana nazo kuwa ni Ongeza Elimu ya Juu,vyama vya siasa na watu binafsi mfano Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta na Prof. Issah Shivji.
Alisema kuwa kwa Zanzibar walipewa ratiba ya kutembelea miradi ya Tasaf, ofisi ndogo ya Bunge na ofisi ya Makamu wa Rais, na kwamba walilalamika kubadilishiwa ratiba hiyo wakiwa Zanzibar.
“Tuliambiwa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah tungepewa fedha za kukaa Zanzibar hata kwa wiki nzima, na tulilipwa fedha nyingi tofauti na tunavyolipwa kwa utaratibu wa kawaida,” alisema.
Lissu alisema kuwa Kikwete aliwahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilishirikishwa, lakini Waziri wa Sheria wa Zanzibar alisema kuwa walipelekewa muswada na Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Wiliam Lukuvi na kuwataka watoe maoni siku hiyo hiyo.
Kwamba Wazanzibari waliona mambo manne waliyopelekewa katika muswada wa mabadiliko ya sheria hayakuwa na shida wakasema sawa, lakini muswada uliopelekwa bungeni ulikuwa na mambo zaidi ya 11.
“Je, hapa kuna uzandiki? Unafiki uko wapi? Je, na waziri huyo wa Zanzibar naye ni mwongo?” alihoji.
Aliongeza kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake alisema ‘ameambiwa’, ‘ameelezwa’ na ‘amefahamishwa’, maneno ambayo ameyatamka mara tisa, na hivyo kuhoji inakuwaje rais anahutubia taifa kwa maneno ya kuambiwa ambayo kisheria hayana nguvu?
“Rais ana uwezo wa kukataa muswada na ana mamlaka ya kukataa mambo ya kijinga yanayopitishwa na wabunge. Tunaomba asisaini muswada huo.
“Rais wetu afanye kama Obama aliyenukuliwa siku za hivi karibuni akisema wabunge wakipitisha mambo ambayo hayana tija kwa taifa hatasaini,” alisema.
Akizungumzia athari za haraka kama rais atasaini muswada huo, Lissu alisema nchi itapata katiba mbovu ya hovyo na matukio ya vurugu kama ya Zimbabwe na Kenya yatajitokeza Tanzania.
Alisema kuwa nchi hizo zilifikia hapo baada ya serikali kujidai inahodhi muswada wa katiba, ikijipendelea yenyewe badala ya kusikiliza wananchi waseme.
Kuhusu wadau ambao waliwasilisha majina halafu rais akateua kadiri alivyoona bila kuteua majina hayo, Lissu alisema hayo hayakuwa mawazo yake, bali waulizwe mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Dk. Charles Kitima na Mchungaji Rohho wa CCT.
Kwa wawakilishi wa Shirikisho la Vyama Vya Wenye Ulemavu (Shivyawata), Lissu alidai kuwa walisema kuwa Alshaymar Kweygir, rais ndiye anajua alivyomteua kwani hawakumpendekeza.

No comments:

Post a Comment