Friday, October 18, 2013

Chadema Mvomero yatoa Tamko na kuwalipua Ma-Rais Wastaafu.

Na Bryceson Mathias,
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Mvomero kimetoa Tamko kali, huku kikiwalipua Ma-Rais wastaafu na watendaji wake wa awamu zilizopita, kikiwataka waachie Ardhi na maeneo makubwa waliyohodhi kuwa ndiyo yanaosababisha Vurugu na Uvunjifu wa Amani baina ya Wakulima na Wafugaji.
Pia, kimeitaka Serikali iachie Ranchi zote za Taifa kilizoshindwa kuziendeleza na badala yake kiwakabithi wafugaji na maeneo ya Kilimo waachiwe wakulima walime ili kurudisha Mshikamano uliokuwepoi kati ya makundi hayo ambayo sasa uhusiano wao mkoani Morogoro umepalaganyika, kilichopo ni vifo kila leo.
Wakitoa Tamko hilo Jana katika kikao cha dharura kilichoketi Ofisi Kuu ya Manyinga wilayani Mvomero, Mwenyekiti wa Chadema, Saimanga Kashikashi alisema, kimefikia kutoa Tamko hilo kufutia Serikali kupiga Chenga kutatua Mgogoro wa wakulima na Wafugaji, na kuwapiga Changa la Macho kwa Vitisho.
“Tunawataka Ma-Rais wastaafu, Ally Hassan Mwinyi, Benjamini Mkapa, Watendaji wa Awamu zao, Viongozi na Watendaji wa Awamu ya Nne, waachie Ardhi na Mashamba makubwa waliyohodhi kwa kuwa ndiyo kiini kinachosababisha Vurugu na Uvunjifu wa Amani baina ya Wakulima na Wafugaji.
“Pande zote mbili zina haki zake, Wakulima wana Haki yao na Wafugaji wana haki yao, hivyo badala ya Wakulima na Wafugaji kufukuzwa katika maeneo yao na Vigogo kujimilikisha maeneo makubwa huku wakiacha sehemu kiduchu wanyang’anyane (wakulima na wafugaji), ambapo Chadema inawataka waachie Ardhi”.
Wakati huo huo wananchi walioshinda Mkindo tangu asubuhi hadi Jioni wakimsubiri Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera, aongee nao kama alivyojipa Kitanzi cha ahadi RPC wa Mkoa, Faustine Shiliogile 14.10.2013 kuwa atampeleka, walisema, Serikali imewapiga Changa la Macho, na badala yake wamepelekewa Vitisho na wajumbe walioitwa wilayani Mvomero.
Katika hali isiyo ya kawaida, Mwenyekiti wa Chadema wilayani Mvomero Kashikashi aliyepita na kuwaamkua wananchi hao akiwa amefunga Bendera ya Chadema kwenye Pikipiki, alishangiliwa na kundi la watu wakipiga kelele
“Haki ya Kweli Iko Chadema na si Chama cha Mapinduzi (CCM)…Hata Bendera ameshindwa kutatua Mgogoro wetu na Wafugaji….Hukumu yao iko 2014-2015”.walisema wananchi hao kwa mayowe.
Hata hivyo Katika kikao na Wawakilishi hao, Mkuu wa Mkoa Bendera alizionya Pande zinazohasimia kwamba, ‘hataki kuona mtu akifunga barabara wala mtu kuvamia eneo la mwenzake kwa visingizio vya aina yoyote ile, kwa kuwa Kesi iko mahakamani, jambo ambalo wakulima wametafsri wanaonewa.

No comments:

Post a Comment