Sunday, September 8, 2013

Sugu aipagawisha polisi

Wahaha kutafuta `wataalamu elekezi` wa kisheria
Mnyika: Naibu Spika naye aadhibiwe, alivunja kanuni
Polisi mkoani Dodoma imekwepa kuzungumzia hatua itakayochukua dhidi ya Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, kwa kosa la kumshambulia polisi, baada ya kutokea tafrani bungeni juzi.
Badala yake, imesema licha ya Sugu, kuhojiwa baada ya kujisalimisha mwenyewe, polisi sasa italazimika kuwatafuta wataalamu wa sheria kusaidia kuamua hatua za kuchukua dhidi ya mbunge huyo anayelindwa na kanuni za kinga ya Bunge, lakini pia akituhumiwa kufanya jinai ya kumpiga polisi.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Suzan Kaganda alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuangalia mazingira halisi ya tukio hilo.
Alhamisi wiki hii, Mbilinyi aliripotiwa kutafutwa na polisi baada ya kutokea vurugu ndani na nje ya Bunge, akidaiwa kumpiga polisi baada ya kutolewa kwa nguvu ndani ya ukumbi huo.
Vurugu hizo zilianza kufuatia kitendo cha Naibu Spika Job Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe , kwa kile alichoeleza kushindwa kutii mamlaka ya kiti cha Spika.
Kamanda Kanganda alisema kwamba Mbilinyi aliachiwa juzi baada ya kuhojiwa na kutimiza masharti ya dhamana.
Alitaja masharti hayo ni kuwa na wadhamini wawili raia wa Tanzania, ambapo mmoja awe mkazi wa mji Dodoma.
Hata hivyo, alisema wakati kazi ya upelelezi inaendelea, mbunge huyo ameagizwa kuripoti kituoni hapo Jumatano ijayo saa 2:00 asubuhi.
Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, John Mnyika, alisema mbunge huyo alijisalimisha mwenyewe juzi saa 11 jioni akiwa na mwanasheria wake Tundu Lisu pamoja na Mbowe na kuhojiwa hadi saa 3:00 usiku.
Akizungumzia suala hilo, Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo, alisema yeye na mwalimu wa shule moja mkoani hapo aliyemtaja kwa jina moja la Mkotya wamemdhamini.
Alisema kwenye maelezo ya Sugu aliyotoa polisi, alieleza jinsi askari na wana usalama walivyomshambulia kwa ngumi na mateke na kuomba wachukuliwe hatua kwa kufanya makosa ya jinai dhidi yake.
"Mimi nimetajwa kama shahidi kuwa nimeshuhudia akielekezwa Sugu atolewe na kupigwa," alisema
Katika hatua nyingine, Mnyika alisisitiza kwamba anakusudia kuchukua hatua za kibunge dhidi ya waliongizwa ndani ya Bunge na Naibu Spika Ndugai kinyume cha kanuni na kutenda makosa ya jinai ya kushambulia wabunge akiwemo Mbilinyi.
Alisema polisi hawapaswi kuendelea kutumika katika jambo hili .
Mnyika alisema kanuni ya 76 ya Bunge inaagiza kuwa kukitokea fujo bungeni Spika anapaswa kusitisha shughuli za Bunge ndipo amwite mpambe wa bunge kuzituliza.
Alieleza kuwa Naibu Spika, hakutumia kanuni hii , hakusitisha shughuli za bunge kabla, hivyo asingeweza kuita askari kuingia ndani mbali na wapambe wanaovalia sare rasmi
“Itakumbukwa kwamba siku zote bungeni watu wengine wakitaka kuingia kama ilivyotokea kwa Taifa Stars au wanafunzi ni lazima kwanza kutengua kanuni za bunge linaloendelea.”
Ilitaja kuwa wanaoitwa ni wapambe wa bunge lakini Naibu Spika aliwaamrisha askari kinyume na kanuni na matokeo yake waliingia hadi wana usalama na wengine wasiohusika wasiokuwa na sare rasmi.
Aliongeza kuwa Naibu Spika naye anastahili kuchukuliwa hatua kwa kuvunja kanuni pamoja na askari na wengine wasiokuwa wabunge walioingia ukumbi siku hiyo.
Mwanasheria maarufu (jina linahifadhiwa) alipohojiwa kuhusu sakata hilo alisema kitendo cha askari hao kumpiga mbunge Sugu bungeni ni udhalilishaji na kuongeza kuwa Sugu naye hakutakiwa kumshambulia askari kwani kufanya hivyo ni kujichulia sheria mkononi.
Alisema wote wana makosa na suala lililopo katika tukio hilo ni kuangalia sheria gani itatumika kuwaadhibu , hata hivyo, alikumbusha kuwa Bunge lina sheria na kanuni zake zinazotakiwa kutumiwa kuhusiana na jambo hilo.

No comments:

Post a Comment