NDUGU zangu,
Kwenye Gazeti la Daily News ya jana, kuna habari hyenye kuhusiana na Muswaada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ukiyaangalia yaliyotokea ndani ya Bunge hivi majuzi na hatimaye muswaada husika kupitishwa kama ulivyopitishwa jana, basi, kwa mtazamo wangu, ninachokiona ni kuwa, inahitajika busara ya ziada kuokoa jahazi la Katiba kuzama.
Maana, haionekani vema kwa Muswada kupitishwa ukishuhudiwe na wabunge watatu tu wa upinzani. Wengine wote wameususia.
Na hapa ninayemwona anaweza kuingilia kati na kuokoa jahazi hili ni Rais mwenyewe; Jakaya Kikwete.
Maana, watu wazima tukubali kuwa pamoja na kupitishwa muswada husika, nyuma yake umeacha manung’uniko yatakayosalia kwa miaka mingi na hivyo basi, kutia doa kubwa mchakato huu mwema ambao rais wetu aliuasisi, akausimamia na umeleta matumaini ya kufungua ukurasa mpya kwa nchi yetu kwa miaka mingi ijayo.
Maana nahofia pia, kuwa ni heri kuwamo kwenye jahazi hili Wazanzibari wengi walioridhia kuliko Wazanzibari wengi wenye manung’uniko. Wenye kunung'unika wanaweza kutoboa jahazi na chombo kikazama. Na wao wenzetu wanaweza kuamua kuogelea kivyao.
Hivyo basi, hayo yenye kufafanulika yafafanuliwe, kwa uwazi, na hata ikibidi, kwa muswada kurudishwa tena bungeni kabla ya Rais kuusaini ukawa sheria. Kama tumetoka mbali kwenye safari yetu hii, ni kwa nini basi tuogope kusimama na kurudi nyuma kidogo ili tuinyoshe njia yetu iliyopinda.
Tuchukue mfano, lile la vurugu mechi ya majuzi bungeni lingeweza kuepukwa kama Spika Ndugai naye angeliendea kwa taratibu na bila jazba. Maana, waliotaka kuongea wangeongea.
Na kama kuna aliyekaidi jambo Spika angemwacha na kumpa adhabu ambayo ingeanza kutumika katika vikao vilivyofuatia. Na kukaidi kwa mhusika kungekuwa na maana tu ya mhusika kupoteza kisiasa badala ya kupata zaidi, maana, adhabu ingefuatia, na jambo lisingekuwa kubwa vile la mpaka kuitwa polisi ndani ya ukumbi wa Bunge. Na polisi wale wangefanyaje maana nao wamejiona wako kwenye shinikizo.
Hakika, yaliyotokea ndani ya Bunge ni mambo ya aibu na wananchi tusingependa kuyaona tena. Hata kama yanafanyika kwa wengine, lakini si utamaduni wetu.
Na hili la nafasi ya Spika na yanayotokea bungeni linasisitiza umuhimu ambao tayari Tume ya Warioba imeshauona, wa kuwa na Spika na naibu wake wasio wanachama wa vyama vya siasa.
Maana, ni vigumu pia kwa spika, ambaye pia ni mbunge, kwenda kinyume na matakwa ya chama chake. Anahitaji kuwa na ujasiri wa kuwa na misimamo yake. Na hatari yake, hutokea kwa spika hata kuonekana anajipendekeza kwa chama chake.
Naam, bado tuna nafasi ya kurekebisha kasoro iliyojitokeza kwenye safari hii muhimu kwa nchi yetu. Safari ya kutengeneza Katiba Mpya kwa miaka 50 na zaidi ijayo. Hivyo basi, ni safari inayotutaka kutoangalia masilahi ya vyama na watu, bali ya taifa.
Mungu Ibariki Tanzania.
Na Maggid Mjengwa
No comments:
Post a Comment