Tuesday, September 10, 2013

Mnyika amkumbusha JK mkutano wa maji

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, amemkumbusha Rais Jakaya Kikwete, kutekeleza ahadi yake aliyoitoa Machi, mwaka huu kuwa angekutana na wadau wote kujadili na kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la maji jijini Dar es Salaam.Mnyika aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa mtaa wa Mavurunza, Kata ya Kimara, Jimbo la Ubungo mwishoni mwa wiki.
Alisema sasa ni takriban miezi saba tangu Rais Kikwete atoe ahadi hiyo mbele ya wananchi waa Golani jimboni humo alipofika kuzindua daraja ambapo wananchi walitoa kilio cha tatizo la maji.
"Katika hili suala la tatizo la maji, naomba tuzidi kuunganisha nguvu zetu sote. Hakuna simile maana maji ndiyo uhai wetu. 
Hakuna mbadala wa maji kama yakikosekana au kutoka kidogo. Mtakumbuka mwezi Machi tulipokuwa hapo jirani Golani kwenye uzinduzi wa daraja, Rais Kikwete aliahidi kuwa tungekutana Ikulu kufanya kikao na kupata ufumbuzi wa tatizo hili,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa iwapo serikali itatekeleza ushauri wa kugawanya kandarasi ya ujenzi wa bomba la maji kama ilivyofanya kwa bomba la gesi kutoka Mtwara, wananchi wa Ubungo na Dar es Salaam kwa ujumla wataondokana na kero ya maji ambayo imekuwa ikiwakabili kwa muda mrefu sasa.
Alisema kuwa utatuzi mwingine kama moja ya suluhisho la muda mfupi wakati wananchi wakisubiri suluhisho la muda mrefu, ni serikali kuunganisha mifumo ya maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ili isaidiane pale ambapo mfumo mmoja unakuwa na upungufu wa maji au tatizo lolote kubwa.

No comments:

Post a Comment