Tuesday, September 10, 2013

Lema: Viongozi wa dini tuombeeni

MBUNGE wa Arusha mjini Godbles Lema amewaomba viongozi wa dini nchini kuwaombea viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuliombea taifa katika kipindi hiki kigumu cha mchakato wa katiba mpya ambayo imeanza kuleta shida.
Lema alitoa ombi hilo juzi mjini hapa katika harambee iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Frandis Ksavery Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Parokia ya Olosipa, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Naomba mtuombee kwani tumedhamiria kuwapigania wanyonge ndani na nje ya Bunge na hatujali majina yoyote tutakayoitwa kwa kuwa tunaamini lengo letu ni kuwakomboa Watanzania hivyo kama tutaitwa majina mabaya kwa lengo hilo basi na tuitwe,” alisema Lema.
Katika Harambee hiyo, jumla ya sh milioni 43, zilipatikana ambapo Lema na marafiki zake walichangia sh milioni 10.
Fedha hizo zilizopatikana ni sehemu ya sh milioni 120 zinazohitajika kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya padri wa kanisa hilo ambaye hivi sasa anaishi katika nyumba ya kupanga.
Awali akizungumza kabla ya kuanza kwa harambee hiyo, Kaimu Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki, Arusha Padri Simoni Tengesi, alisema mbali ya ujenzi wa nyumba hiyo, kanisa lake lina mpango wa kujishughulisha na huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali na huduma nyingine za wananchi wote bila kujali madhehebu yao.

1 comment:

  1. Kuombea amani nchi ni sawa lakini ninyi wanasiasa wa vyama vyote,tunatakiwa tuwaombee ili,mbadilike na kuwa wakweli zaidi ya kututumia wananchi kwa maslahi yenu binafsi,hivi uni aibu kutumia mikutano ya dini kueleza mambo yasioendana,Tanzania tuko huru toka 1961,sasa huu ukombozi unaonadi ninyi ni upi kama sio uzushi mtupuu.Hebu tueleze wewe kama Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini,unasimamiaje fungu la matibabu kwa Kina Mama wajawazito na Watoto wenye mri wa chini ya miaka mitano,maana kila kukicha hili kundi halipati tiba ya bure,sasa nalo hili nahitaji mpaka mchukue nchi ili hali lipo ndani ya uwezo wenu.Hebu Muogope Mungu ndugu,tumikia wananchi wako badala ya kunadi ukombozi wa uongo.

    ReplyDelete