Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba hautafika mbali hata kama wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitumia uwingi wao bungeni kuupitisha na kwamba kuendelea kulazimisha suala hilo kunaweza kusababisha machafuko nchini.
Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha NIPASHE, kinachorushwa na Redio One, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema wabunge wa CCM na viongozi wa serikali lazima watambue kuwa katiba ni jambo la maridhiano si jambo la kulazimishana.
“Wabunge wa CCM wanaweza kutunga sheria na muswada wanayotaka sababu wapo wengi lakini lazima waelewe kwamba kutumia wingi wao kulazimisha jambo muhimu kama la katiba ni kuweka machafuko ndani ya Taifa,”alisema.
Mbowe alisema mchakato wa katiba unahitaji hekima na busara sana lakini mambo yanayofanywa na CCM ni wazi kuwa muswada huo hautafika salama.
“Tunawataka na tunamuomba Rais na viongozi wengine wa CCM ambao pengine wana hekima kuliko hata wale waliopo ndani ya bunge watumie fursa hiyo kutafuta namna ya kufikia mwafaka katika masuala ya katiba,”alisema.
Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alisema hivi sasa zipo taarifa kuwa wanaharakati ambao ni kundi lililopo nje ya wanasiasa wanajipanga kwenda mahakamani kupinga sheria ya marekebisho ya katiba iliyopitishwa wakati wa mkutano wa 12 wa bunge.
Alisema Naibu Spika Job Ndugai hakuweza kuheshimu nafasi yake (Mbowe) kama kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni kwa kukataa kumpa nafasi ya kuzungumza jambo ambalo ni kinyume cha kanuni
“Naibu Spika badala yake aliruhusu askari kuingia bungeni wakaanza kupiga wabunge, kutumia nguvu ,kutukanwa na mambo ya kudhalilishana, mnategemea hiyo amani ambayo ingeturudisha bungeni kuendeela na mjadala ingetoka wapi,”alisema Mbowe.
Mbowe alisema maamuzi ya kutaka muswada huo ujadiliwe bungeni yalikuwa yamekwisha pitishwa kwenye kikao cha wabunge wa CCM na kwamba hilo ndilo tatizo la kuwa na viongozi wanatoka chama kimoja cha siasa.
Kwa upande wake, Naibu Spika, Job Ndugai alisema wabunge wa kambi ya upinzani walishiriki mjadala wa majadiliano ya Muswada wa Marekebisho ya Katiba licha ya kuonekana wakitoka nje ya ukumbi wa ubunge kwasababu walijiandikisha kwenye kitabu cha mahudhurio na kupata posho ya siku hiyo.
No comments:
Post a Comment