Monday, September 9, 2013

Kibano chamgeukia Ndugai - MZEE MOYO

*Yadaiwa alipewa maelekezo kuwabana wapinzani
*Profesa Lipumba adai uwezo wake bungeni mdogo

NAIBU Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, amezidi kujiweka katika wakati mgumu, baada ya viongozi wa vyama vya upinzani kudai alipewa maelekezo na Serikali kupitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba.
Kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF), walisema ni wazi, Ndugai ameonekana kuwa na uwezo mdogo wa kuongoza Bunge, kutokana na kusababisha vurugu kubwa ndani ya ukumbi wa Bunge wiki iliyopita.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uwezo wa Ndugai kuongoza Bunge unahatarisha amani, mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo sasa kutokana na kutokuwa na mtazamo mpana wa kufikiri.

Alisema mbali ya uwezo, kulikuwa na ajenda ya chini chini kati ya kiti cha Spika, Serikali na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhujumu malengo na nia ya Rais Jakaya Kikwete kuwa na Katiba Mpya ifikapo mwaka 2015.

Alisema kitendo cha Ndugai kuamuru polisi kumtoa ndani ya Bunge Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ni cha aibu na cha kidikteta.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa Serikali (hakuwataja), wanajionyesha wanamsaidia Rais Kikwete lakini ndani ya mioyo yao wana ajenda za siri za kumhujumu.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia udhaifu wa Ndugai kwa kumshawishi kufanya kile wanachoona kinafaa, kwa lengo la kukandamiza upinzani na kumhujumu Rais Kikwete bila yeye kujua.

Alisema kuna kawaida kwa kiti cha Spika hasa kinapokaliwa na Ndugai kuendesha Bunge kwa kuipendelea Serikali kwa kadri kinavyoweza, huku kikizima hoja za upinzani kwa makusudi.

“Kuna njama za wazi zinafanywa na kiti cha Spika kwa kutelekeza maoni ya wananchi na kupendelea ya CCM, kwa upande wa Zanzibar hawakushirikishwa vizuri na hata wabunge wa CUF wanasema hawakushirikishwa.

“Moja ya njama za wazi ni ile ya wabunge 166 wa Bunge la Katiba wanaopaswa kupendekezwa na taasisi mbalimbali na kuteuliwa na rais, sisi CUF tunasikitishwa na mchakato unavyoendeshwa na jinsi uteuzi unavyopendekezwa.

“Hii Katiba Mpya itakuwa ni ya CCM si ya Watanzania, na ombi la wabunge wa CUF ni kutaka muswada urudishwe kwa wananchi na kamati ijadili upya,” alisema Profesa Lipumba.


CHADEMA
Katika hatua nyingine, CHADEMA kimesema Ndugai alipewa maelekezo na Serikali kukwamisha wabunge wa upinzani.

Akizungumza ofisini kwake Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, alisema ndiyo maana aliruhusu kitendo cha muswada huo kujadiliwa.

Alisema kutokana na kitendo hicho, CHADEMA kupitia sekretarieti yake, imeitisha mkutano wa dharura utakaoshirikisha vyama vingine vya upinzani na wadau wa Katiba, utakaoongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, kujadili suala hilo na hatua za kuchukua kuanzia leo.

“Kwa kitendo hiki, Naibu Spika amekiuka mila na desturi za kibunge, akaenda mbali zaidi akavunja kanuni ya 76.

“Kifungu hicho kinasema kwa madhumuni ya kudhibiti fujo endapo itatokea ndani ya ukumbi wa Bunge na Spika ataona kuna haja ya kutumia nguvu, basi anaweza kuahirisha shughuli za Bunge bila ya hoja yoyote kutolewa au kusitisha kikao kwa muda atakaoutaja ili fujo hiyo iweze kudhibitiwa na mpambe wa Bunge.

“Baada ya utulivu, Spika atalipeleka kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, suala ambalo lilisababisha kutokea kwa fujo, ikiwa ni pamoja na jina la mbunge au majina ya wabunge waliohusika na fujo hiyo ili kamati iweze kulishauri Bunge kuhusu adhabu inayostahili kutolewa.

“Lakini pia katika kanuni ya tano (1), inasema katika kutekeleza majukumu yake yaliyotajwa katika ibara ya 84 ya Katiba, Spika ataongozwa na kanuni hizi na pale ambapo kanuni hazikutoa mwongozo, basi Spika atafanya kazi kwa kuzingatia Katiba, sheria nyingine za nchi, kanuni nyingine zilizopo za mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na utaratibu wa Bunge la Tanzania.

“Kitendo cha Spika kuagiza watu watolewe ni kinyume na kanuni za Bunge, alitokea mtu anaitwa Peter Magati, yeye si mpambe wa Bunge, maana hao ndiyo kimsingi wenye kazi hiyo, inaonyesha wazi yale yalikuwa ni maelekezo maalumu,” alisema Mnyika.

Alisema katika mkutano huo, pia watajadili ushauri waliopewa na watu wengine waende mahakamani kushinikiza Rais Jakaya Kikwete asisaini muswada huo ili usianze kazi na urudi bungeni kujadiliwa upya, kumpigia kura Ndugai ya kutokuwa na imani naye au kumfikisha katika Kamati ya Haki, Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Sisi tafakari yetu ya kwanza ni kurudi kwa wananchi, hii ndiyo mahakama yetu na huu ni wakati wa madaraka ya mamlaka ya wananchi kutumika.

“Katika mazingira kama hayo, ili tuiokoe nchi katika uchaguzi mkuu ujao na kuepusha vurugu za uchaguzi kama zile zilizotokea nchini Kenya mwaka 2007, lazima kufanyike marekebisho ya Katiba kwenye maeneo yanayohusu uchaguzi ili uwe huru na wa haki kuanzia Serikali za Mitaa hadi uchaguzi mkuu,” alisema Mnyika.
MZEE MOYO
Kwa upande wake, mwanasiasa mkongwe visiwani Zanzibar, Hassan Nassoro Moyo, amesema wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, wamewasaliti Wazanzibari kwa kushindwa kuungana na wabunge wa CUF kutetea ushiriki wa Wazanzibari katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Muswada huo uliopitishwa bungeni juzi na wabunge wa CCM pekee, huku wabunge wa Kambi ya Upinzani wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, wakidai Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge, haikushirikisha wadau wa Zanzibar kutoa maoni yao.

Akizungumzia hali hiyo, Mzee Moyo, aliwalaumu wabunge wa Zanzibar akidai wameonyesha udhaifu mkubwa kwa kuweka mbele maslahi ya chama chao kuliko wananchi wa Zanzibar.

“Kilichotokea bungeni ni fitina za vyama vingi, wameweka mbele maslahi ya vyama vyao kuliko maslahi ya wananchi, wanastahili kulaumiwa.

“Ni kwanini hawa wabunge wa Unguja wameshindwa kuungana na wenzao wa CUF kutetea maslahi ya Zanzibar, ndio maana Mzee Karume mwaka 1952 alikataa vyama vingi aliamini vyama vingi ni fitina tu,” alisema Mzee Moyo.

Alisema anaamini wapo baadhi ya watu serikalini wamejenga chuki na dharau kwa wajumbe wa kamati yao na kusisitiza kamati hiyo haitorudi nyuma kupigania maslahi ya Wazanzibari.

Akizungumzia msimamo wa Serikali tatu unaoungwa mkono na kamati yake, Mzee Moyo, alisema anakubaliana na msimamo huo, huku akisisitiza wakati umefika kuwapo na Serikali ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment