ADAI WALISHINIKIZA AFUNGULIWE KESI YA KUVULIWA UBUNGE
BAADA ya Mahakama ya Rufaa kuafiki ombi la wakili Godfrey Wasonga la kuondoa kesi ya kupinga ubunge wa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), mbunge huyo ametangaza kusudio la kuwashtaki Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mtangulizi wake Yusuph Makamba.
Katika kesi hiyo ambayo atamuunganisha pia wakili wa CCM, Wasonga na bodi ya wadhamini ya chama hicho, Lissu anadai kuwa viongozi hao ndio walishinikiza afunguliwe kesi ya kupinga ubunge wake.
Katika Mahakama ya Rufani jana, jopo la majaji watatu, Salumu Massati, Engela Kileo na Natalia Kimaro, liliridhia ombi la wakili Wasonga kuondoa kesi hiyo mahakamani kwa sababu kuwa waliokuwa walalamikaji, Shaban Selema na Paskali Hallu, walijitoa wote wakisema hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
Awali kulikuwa na ubishani mkubwa wa kisheria kuhusu uhalali wa kesi hiyo kuondolewa mahakamani, ambapo mlalamikiwa namba moja, Tundu Lissu, alisema kuwa maombi hayo ya kuiondoa yalikuwa yameletwa kwa nia mbaya ili kuifanya mahakama isitende haki.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wakili wa serikali, Vincent Tango, na kuongeza kuwa hata ombi hilo lilikuwa limewasilishwa kinyume cha sheria.
Akisoma uamuzi wa mahakama, Jaji Kileo alisema baada ya kuangalia mazingira ya kesi yenyewe na kwa namna walalamikaji walivyojitoa, mahakama haikuona sababu ya kumwambia wakili Wasonga alipe gharama kama Lissu alivyoomba.
Badala yake mahakama iliamuru mlalamikaji wa pili katika kesi hiyo aliyechelewa kujitoa mpaka kesi ikapangwa kusikilizwa, ndiye alipe gharama za kesi hiyo, huku gharama za kesi katika mahakama kuu wazilipe na waliokuwa walalamikaji wote wawili.
Akizungumza na gazeti hili baada ya uamuzi huo, Lissu alisema sasa anawashtaki viongozi wa CCM kwa kushinikiza afunguliwe kesi bure.
“Ninao ushahidi wa maandishi jinsi Makamba na Kinana walivyokuwa wanashinikiza na kusaidia kulipa fedha ili mimi nifunguliwe kesi,” alisema.
Lissu alisema atamshtaki Makamba kwa kuwa aliagiza yeye ashtakiwe na Kinana alikuwa anashinikiza rufaa ikatwe licha ya walalamikaji wote kujitoa tangu awali.
Hata hivyo Lissu alisema rufaa hiyo haikupaswa kukatwa, kwani Aprili 27, 2012, ndio hukumu ilitolewa Singida na Jaji Moses Mzuna ambapo kwa taratibu za kisheria walipaswa kutoa taarifa ya kukata rufaa ndani ya siku 30 na kuwapatie walalamikiwa taarifa hiyo.
“Hadi rufaa inatajwa na hukumu kutolewa sijawahi kupatiwa notisi hizo za rufaa wala nakala ya hukumu, na mwenendo wa kesi kama waliamua kutokutoa taarifa walipaswa kukata rufaa ndani siku 60, lakini rufaa tunayosikiliza leo imekatwa Mei 20, 2013.
“Kisheria rufaa hii haikupaswa hata kupokelewa na mahakama na kama walifungua kwa kuchelewa kisheria barua yao ya maombi ilipaswa kusainiwa na Msajili wa Mahakama ili kueleza sababu za kuchelewa,” alisema.
Aliongeza kuwa alishangaa kwani licha ya kasoro hizo, hicho kinachoitwa hati ya msajili alichopewa hakina jina la msajili wala sahihi na muhuri wa mahakama ingawa rufaa imepangiwa tarehe na imesikilizwa.
Lissu alisema kuwa kesi yake kukatiwa rufaa mwaka huu ni baada ya hotuba ya upinzani kumtaja Kinana kuwa kinara wa biashara ya pembe za ndovu.
“Ndipo Kinana alianza mpango wa kuwasiliana na wakili Wasonga kumshauri akate rufaa na kuahidi kuwalipa majaji kila mmoja sh milioni 300 ili ubunge wangu utenguliwe,” alisema.
Tanzania Daima lilipata barua ya tarehe 20/05/2013, yenye kumb.No/KM/CCM/01/2013 kutoka kwa Wasonga kwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu maandalizi ya rufaa Mahakama Kuu yanahitaji gharama kubwa sana, hii ni kutokana na umakini unaohitajika na pia kuwalipa watu wa kufanya kazi husika, hivyo naambatanisha invoice ya malipo ya awali ya sh 2,000,000 fedha za maandalizi ya awali ya sababu za rufaa pamoja na vitabu husika.
“Ikumbukwe kuwa katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM mkoa wa Singida na hawakumaliza malipo, CCM Daima kurudi nyuma mwiko,” ilisomea batua hiyo.
Barua hiyo ya Wasonga kwenda kwa Kinana iliambatanishwa na invoice namba 076, yenye TIN 109-920-649 ili Kinana alipe malipo hayo ya rufaa.
Kwa mujibu wa Lissu bila Makamba na Kinana, asingefunguliwa kesi hizo za bure.
“Sasa nitawashtaki na wakili wao pamoja na bodi ya wadhamini wa CCM, na watanilipa ili nipate fedha za maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015,” alitamba.
Baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010, CCM kupitia kwa Makamba, iliandika barua yenye kumb. Na. CCM/OND/636/VOL.11/122 ya Novemba 9, 2010 kwenda kwa makatibu wake wa mikoa na wilaya kuwaamuru wote walioshindwa katika uchaguzi wapinge matokeo na kwamba chama kingewasaidia gharama za uendeshaji wa kesi hizo.
Katika barua hiyo, Makamba aliwataka wagombea wa ubunge kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, huku wagombea udiwani walioangushwa kufungua kesi katika mahakama za hakimu mkazi ndani ya siku 30, tangu ulipofanyika uchaguzi huo.
Sugu amponza ofisa
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Upelelezi wa Dodoma mjini, Jumanne Amasi, ameingia matatani na kulazimishwa kuhamia Iramba ili yule wa Kiomboi aende Dodoma kuisaidia CCM kukabiliana na wapinzani.
Taarifa kutoka chanzo chetu zimethibitisha kuwa mkuu huyo wa upelelezi amehamishwa kwa dharura kwenda Iramba kutokana na shinikizo la kigogo mmoja wa CCM.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kutokana na mkuu huyo kukataa maelekezo ya kigogo huyo yaliyomtaka amweke mahabusu mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), baada ya fujo zilizotokea bungeni.
Inadaiwa kuwa awali mkuu huyo pia alikataa kumkatama Mbilinyi maarufu kama Sugu alipokuwa Desert Hotel ya mjini Dodoma, akitoa sababu kwa wakuu wake kwamba kosa la mbunge huyo lilitendekea bungeni na alipaswa kuwajibishwa kwa kanuni za Bunge.
Alipotafutwa msemaji wa polisi kwa simu kufafanua madai hayo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Chanzo chetu kimethibitishiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Iramba kuwa tayari amepokea taarifa za kuhamia Dodoma kikazi lakini akadai ni masuala ya kawaida.
Naye mkuu wa upelelezi wa Dodoma, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwani alidai kuwa hana taarifa na kwamba kama atahamishiwa Iramba atachukulia kama sehemu ya kazi.
Mh. Lisu usiache kuvuta hio hela kutoka kwa hao mafisadi,Makamba gafla ni tajiri na Kinana tembo wakisikia tu harufu yake wanachanganyikiwa.Pia tafuta na namna ya kumuunganisha billionea William Vangimembe Lukuvi ambaye amenunua jumba la kifalme pale Mbezi beach,mtaa wa Colonel Mitha, jirani na kanisa la wakorea la Good News Mission, kwa million 700 taslim akalibomoa na kulikarabati kwa zaidi ya billion moja.Alitaka kuhamia kwa mbwembwe wiki tatu zilizopita lakini akanywea baada ya paparazi kutia timu hapo na wengi kumhoji Lukuvi kama ni kipato chake halali na kwa nini anagwaya kuwataja wabunge anaodai wanauza madawa ya kulevya?
ReplyDelete