Saturday, September 14, 2013

Lissu aibwaga CCM

Mahakama yaamuru alipwe gharama zote
Yamtangaza mbunge halali Singida Mashariki
MAHAKAMA ya Rufani Tanzania, imekubaliana na ombi la kutupiliwa mbali rufani ya kutengua hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, iliyomthibitisha Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) kuwa ni mbunge halali.

Mbali na hilo, pia mahakama hiyo imewaamuru warufani, Shabaan Selema na Paschal Halu, kulipa gharama zote zilizotumika kuendeshea kesi hiyo katika Mahakama Kuu.

Mrufani wa pili, Halu, ametakiwa kulipa gharama za kesi kwa upande wa Makakama ya Rufani, kutokana na kuchelewa kupeleka taarifa za kutokuwa na nia ya kuendelea na rufaa hiyo, wakati shauri hilo likiwa limeshapangwa.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya warufani wote kujitoa katika kesi hiyo namba 49/2013, ambayo ilipangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, wakiongozwa na Jaji Engela Kileo, pamoja na Salumu Massati na Natalia Kimaro.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Kileo alisema mahakama hiyo imekubaliana na ombi la kuondoa rufani hiyo mahakamani kwa kanuni ya 4(a) na (d) za Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009.

Awali wakili wa warufani hao, Godfrey Wassonga, aliwaambia majaji kwamba hawawezi kuendelea na kesi hiyo kutokana na wateja wake kujitoa, hivyo alitumia kifungu namba 102 cha Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009 kuomba rufaa hiyo iondolewe.

Akizungumza nje ya mahakama, Lissu alisema hukumu hiyo haijamshangaza, kwa sababu rufaa hiyo haina kichwa wala miguu na ilipelekwa na watu wasiojua sheria.

“Sijashangaa hata kidogo kuwa Mahakama ya Rufaa, imeitupilia mbali, huyo wakili wao ana bahati, vinginevyo alitakiwa kulipa hizo gharama mwenyewe.

“Tunajua analipwa na Kinana (Katibu Mkuu wa CCM), lakini yeye kaamua kufungua tu kesi pamoja na kwamba wahusika walimwambia mapema kwamba hawataki kuendelea na kesi, lakini yeye ameendelea na rufaa kwa sababu tu Kinana amesema,” alisema Lissu.

Kwa upande wake, Wassonga alisema Hukumu hiyo ni ya kawaida na warufani hao watalipa gharama zote za kesi.

Naye mmoja wa warufani hao, Shaaban Selema, akizungumza nje ya mahakama alisema yeye alijitoa katika kesi hiyo baada ya kuona baadhi ya viongozi wa CCM wakiwatumia kwa manufaa yao.

"Mgombea mwenyewe aliyekuwa akiitwa Jonathan Jau alinikashfu katikati ya mwezi wa pili, nikaamua kujiunga na Chadema," alisema.

Alisema ameridhishwa na hukumu hiyo na kama itafika mahala wakawa wanadaiwa, basi wale waliowashauri kuingia kwenye kesi watawaambia walipe.

"Kuhusu gharama tutaangalia nani ana haki ya msingi ya kulipa, huyu mwenzangu ndo analipia, atajua mwenyewe kama atasaidiwa na Kinana au na CCM," alisema Mrufani huyo.

No comments:

Post a Comment