Saturday, August 3, 2013

Rasimu yawaondolea sifa wanaowania urais

Rasimu ya katiba mpya inayoendelea kujadiliwa inaashiria kuwaondolea sifa za kuchaguliwa kuwa rais idadi kubwa ya wanasiasa wanaoonyesha nia ya kugombea wadhifa huo.

Katika rasimu hiyo, kipo kipengele kinachoeleza kuwa mgombea atachaguliwa kuwa mbunge ama rais iwapo hajawahi kushika wadhifa wa ubunge kwa zaidi ya vipindi viwili.

Angalizo hilo limetolewa na mwanasiasa mkongwe nchini , Arcado Ntagazwa. Bila kuwataja aliwashauri wagombea hao wanaoendesha kampeni za kuwania urais kuisoma na kuielewa rasimu wakati wakisubiri katiba itoe mwelekeo wa sifa za kuchaguliwa kuongoza taifa.

Ntagazwa ambaye anaheshimika kama mwanasiasa mtiifu kwa falsafa za Mwalimu Nyerere, ni mmoja wa viongozi waliokubali mabadiliko na siasa za vyama vya ushindani ambaye licha ya kuwa kada wa CCM, ni mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Aliwaasa kuwa si wakati wa kuanza kampeni na kujipa tumaini la urais ambalo mchakato wa katiba mpya haujaeleza hatma yake.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE Jumamosi, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, mwanasiasa huyo alihoji kipengele cha sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge ambazo zinataka mgombea ambaye hajawahi kushika wadhifa huo kwa zaidi ya vipindi viwili kuchaguliwa kuwa mbunge.

“Ninachojiuliza wanataka wabunge wawe wapya kabisa wasio na uzoefu wanaokwenda kujifunza upya ama lengo nini hasa? ” alihoji.

No comments:

Post a Comment