Saturday, August 3, 2013

CCM kwawaka

WAZEE WAKERWA NA KAULI YA NAPE KWAMBA “WANASUBIRI KUFA”
MATUKIO kadhaa ya kisiasa, mwelekeo, kauli na mienendo ya baadhi ya wanasiasa waandamizi na wenye nguvu katika Chama cha Mapinduzi (CCM) vimeibua mkanganyiko na hali tete ndani ya chama hicho, Tanzania Daima Jumamosi limebaini.
Kwa muda sasa, kumekuwa na minyukano ya ndani kwa ndani miongoni mwa viongozi waandamizi wa CCM, huku baadhi yao wakilaumiana kwa “kuchafua na kuua” chama.
Baadhi yao wamefikia hatua ya kumlaumu Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kwa kuwapa madaraka makubwa baadhi yao, na kushindwa kuwanyang’anya pale wanapoonyesha dalili za “kuua” chama chao.
Gazeto hili linazo taarifa za baadhi ya viongozi wastaafu wa CCM kupeleka ujumbe mzito kwa Makamu Mwenyekiti, Phillip Mangula, wakionyesha kukerwa na kauli au mwenendo wa baadhi ya viongozi waandamizi, hasa Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba.
Wanamtuhumu Nchemba kwa kushusha heshima ya CCM mbele ya umma, na kuchangia matokeo mabaya katika uchaguzi wa madiwani uliofanyika Arusha mwezi uliopita, ambako CCM ilishindwa na CHADEMA katika kata zote nne.
Baadhi ya wazee na makada waandamizi wanasema Nchemba ni “mzigo wa Kikwete,” kwa maana kuwa ndiye aliyempa madaraka, na ndiye anayemsikiliza na kumpa jeuri.
Nafasi anayopewa Nchemba imeleta mgongano wa chini kwa chini kati yake na Katibu wa itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye kwa muda sasa amekuwa ndiye kipenzi cha Rais Kikwete katika kutekeleza mikakati kadhaa na kutoa matamko yenye utata dhidi ya viongozi au wanachama “wasiopendwa” ndani ya chama hicho, au dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa makada wanaokerwa na tabia ya Nchemba, kiongozi huyo amegeuka kero kwa viongozi wenzake, ambao wanasema ameingiza siasa za ujasusi wa waziwazi na mbinu nyingine chafu za kisiasa zinazomfanya aibomoe CCM na kuiongezea umaarufu CHADEMA mbele ya umma.
Mbali na mnyukano wa uongozi, Nape amejikuta katika mgogoro mzito na wazee ndani ya chama hicho baada ya gazeti moja kumnukuu akitamka kwamba wanaoshabikia mfumo wa serikali tatu katika kujadili rasimu ya Katiba mpya, ni “wazee wanaosubiri kufa”.
Baadhi ya wazee na makada waandamizi wamekerwa na kauli ya Nape, wakisema inaonyesha jeuri isiyo ya kawaida kwa kijana mdogo kama yeye.
Miongoni mwa wanaodai kukerwa na kauli hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji, Joseph Warioba, na waasisi kadhaa wa CCM wakiwamo Joseph Butiku, Jaji Mark Boman, Dk. Salim Ahmed Salim, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa na wengine, hata wale wasiounga mkono hoja ya serikali tatu.



Hata hivyo, Nape anadaiwa kuwa amepiga simu kwa baadhi ya wazee hao kuwaomba radhi na kukanusha kauli hiyo, akidai kuwa alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari.
Baadhi yao wanasema hata kauli ya majuzi ya waziri mstaafu, Mateo Qaresi, ya kuiponda serikali na uongozi wa CCM, imetokana na hasira dhidi ya kauli ya Nape, ingawa msimamo wake juu ya mfumo wa muungano wa serikali ni ya siku nyingi.
Waziri huyo mstaafu amenukuliwa akisema, “Hivi hawa viongozi wanajua tunakoelekea, leo hii ukiulizwa dira yetu ni nini hakuna anayejua, bali tunajiendea tu,” kauli ambayo imeibua hisia kali ndani ya serikali na CCM.
Qaresi katika utumishi wake wa umma, amewahi kuwa Waziri wa Ushirika na Masoko kati ya mwaka 1989 - 1990, Waziri wa Utumishi, 1996 - 2000 na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya tangu 2000 hadi Februari 2006.
Taarifa kutoka vyanzo kadha vya habari zinasema kauli ya Nape imepunguza makali ya hoja ya CCM kuhusu serikali mbili, na imeongeza hamasa kwa wanaotaka serikali tatu, hasa wenye umri mkubwa ambao Nape amesema wanasubiri kufa.
Kwa sababu hiyo, hata mjadala juu ya Katiba mpya unaelekea kuchukua mwelekeo tofauti kwani hisia hizi zimeanza kuibua makundi pinzani ndani ya CCM, wakati ambapo hoja kuu ya chama hicho ni muundo wa serikali mbili, ambayo sasa imeanza kuwagawa.
Zipo taarifa kwamba baadhi yao wameapa kuwaadhibu kina Nape kwa kuunga mkono hoja ya serikali tatu kwa kishindo, wakidai kwamba ni hitaji la wakati.
Huku CCM wakisisitiza kwamba serikali tatu ni gharama kubwa isiyoweza kubebwa na Watanzania, kina Qares wanasema gharama kubwa zinasababishwa na matumizi mabaya, ufisadi, na taifa kukosa dira.
Qares alisema kwamba hata bila serikali tatu sasa, serikali imetenga kutumia sh trilioni tano (5) tu kati ya sh trilioni 18 za bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14, jambo ambalo linadhihirisha kuwa watawala wanatanua badala ya kuelekeza fedha hizo kwenye maendeleo.

No comments:

Post a Comment