MBUNGE wa Ubungo John Mnyika (CHADEMA), amewasiliana na ofisi ya Bunge na akitaka muswada wa hoja binafsi ya Baraza la Vijana Taifa uchapwe katika gazeti la serikali kwa ajili ya kujadiliwa bungeni.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema sababu ya hatua hiyo ni kutaka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana utakaosimamiwa na vijana wenyewe.
Alisema hatua hiyo inatokana na kuwapo malalamiko ya zaidi ya miaka 15 ya kutokuundwa kwa baraza hilo huku kukiwa na matumizi mabaya ya fedha za maendeleo ya vijana kwenye ngazi mbalimbali ikiwemo katika halmashauri nyingi nchini.
“Ikumbukwe kwamba kwa mara ya kwanza niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge taarifa ya muswada binafsi wa Sheria ya kuunda Baraza la Taifa la Vijana (The National Youth Council Bill, 2013) kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (1) na Taarifa ya Muswada huo kwa mujibu wa Kanuni ya 81 (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la Mwaka 2007) tarehe 4 Januari 2013,” alisema.
Mei 21 mwaka huu, wakati Bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mnyika alitoa hoja ya kuondoa shilingi akitaka serikali iwezeshe muswada binafsi kuchapwa katika gazeti la serikali ikiwa ni maandalizi ya muswada huo kuwasilishwa bungeni.
Katika kikao hicho alitaka ufafanuzi toka kwa serikali kwa mujibu wa kanuni ya 103 (1) kuhusu hatma ya muswada binafsi wa Sheria ya Baraza la Vijana la Taifa.
No comments:
Post a Comment