SERIKALI imesema maoni yaliyotolewa na wadau wa sekta binafisi wakati wa kujadili rasimu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya sekta hiyo yataingizwa katika rasimu hiyo ili kuja na sera mpya itakayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi baada ya kufungua mkutano wa wadau wa sekta binafsi uliokuwa ukijadili mapendekezo ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Sekta Binafsi.
“Kwa mara ya kwanza rasimu hii inajadiliwa na wadau…hii ni hatua muhimu katika kuiwezesha sekta hiyo iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi,” alisema.
Alisema maoni yaliyopatikana katika kikao hicho yataingizwa katika rasimu hiyo, ili kuiimarisha zaidi na baadaye kuletwa kwa mara nyingine kama juhudi za kupata sera bora.
Akifafanua zaidi alisema lengo la kufanya hivyo ni kusaidia sekta binafsi kuzidi kuwa na nguvu na kuingia katika miradi mbalimbali ikiwemo ya madini na gesi.
“Nchi imepata mafanikio makubwa ya maendeleo ambapo uchumi unakua kwa asilimia saba, lakini kazi kubwa inatakiwa kufanyika ili wananchi nao waweze kunufaika na kukua kwa uchumi huu…hii ni njia mojawapo ya kufanikisha hilo,” alisema Dk. Nagu.
Alisema pia sera hiyo itasaidia kufikia dira ya taifa ya maendeleo 2025, Mkakati wa Kupunguza Umaskini na Kukuza Uchumi (Mkukuta), Malengo ya Miaka Mitano ya Maendeleo, Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), Kilimo Kwanza, SAGCOT na Matokeo Makubwa Sasa. Kaimu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Aloyce Mwamanga, alisema kuwepo kwa sera ya taifa ya sekta binasi ni jambo lililokuwa likipiganiwa kwa muda mrefu kwa sababu sekta binafsi ndiyo inayoendesha uchumi.
No comments:
Post a Comment