Saturday, August 17, 2013

Mbowe: Hatutakubali kuibiwa kura tena

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kamwe chama chake hakitakubali kuibiwa kura katika uchaguzi mkuu ujao na chaguzi zingine zozote zitakazojitokeza.

Alisema chama hicho hakitalalamika tena hadharani kuwa kiliibiwa kura katika uchaguzi mkuu uliopita kwa sababu kufanya hivyo ni kuonyesha udhaifu.

“Mimi kama Mwenyekiti nasema lugha ya kukiri kwamba tuliibiwa kura ni udhaifu na ujinga. Mliibiwa kura mkiwa wapi? Nataka niwaambie kuwa hatutaibiwa kura tena labda sisi ndiyo tuibe,” alisema.

Mbowe alitoa kauli hiyo jijini Mwanza juzi wakati wa mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika kwenye uwanja wa Magomeni Kirumba kwa lengo la kutoa elimu na kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba.

Kauli hiyo ya Mbowe ilikuja baada ya kuwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo chimbuko la kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuwa ni matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita ambapo kura za Chadema hazikutosha.

Wakati Mbowe akisema kura za Chadema hazikutosha, wafuasi wa chama hicho walipaza sauti wakidai matokeo yalichakachuliwa.

Hata hivyo, Mbowe aliwaambia wafuasi hao kwamba kuendelea kulalamika kuwa waliibiwa kura ni kuonyesha udhaifu na ujinga.

Badala yake alisema ni jukumu la viongozi, wagombea, wanachama na wafuasi wa chama hicho kuhakikisha kura haziibwi tena katika chaguzi mbalimbali zitazofanyika hapa nchini ukiwamo uchaguzi mkuu ujao.

“Kumbukeni kwamba katika ushindi wa Wenje (Nyamagana), Mnyika (Ubungo), Lisu (Singida Mashariki), Mdee (Kawe), mimi mwenyewe (Hai) na wengine wengi ilibidi yatumike mabomu lakini bado wananchi walilinda kura zao,” alisema.

Aliongeza kwamba kwa kuzingatia hali hiyo haoni sababu yoyote ya chama hicho kuendelea kulalamika hadharani kuwa kiliibiwa kura wakati wana uwezo wa kuzilinda kama ilivyofanyika katika baadhi ya maeneo kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Akizungumzia chimbuko la mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Mbowe alisema kwamba baada ya kutoridhishwa na matokeo katika uchaguzi mkuu uliopita wabunge wa chama hicho waliazimia kususia hotuba ya Rais Jakaya Kikwete ya kuzindua Bunge.

Alibainisha kwamba katika hatua ya kukusanya maoni Tume ya mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba iliweza kuwafikia wananchi 18,000 tu kati ya Watanzania milioni 44.9 huku ikiwa imetumia kiasi cha Shilingi bilioni 20 kati ya bilioni 40 zilizotengwa kwa mchakato mzima. 

No comments:

Post a Comment