Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa anatarajia kuanza ziara ya siku mbili leo mkoani Singida kwa kufanya mikutano kadhaa akianzia wilayani Manyoni kwa kutumia usafiri wa helikopta, maarufu kama 'Chopa'.
Kaimu katibu wa chama hicho mkoa wa Singida, Yahaya Ramadhani, aliyefuatana na katibu wa Chadema wilaya Singida Vijijini, Shabani Limu, aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa Dk. Slaa ataanza ziara hiyo katika jimbo la Manyoni Mashariki na mkutano wake wa kwanza atahutubia kwenye mji mdogo wa Itigi.
Alisema siku hiyo hiyo atafanya mkutano mwingine wa pili makao makuu ya wilaya Ikungi, kabla ya kuelekea jimbo la Iramba Mashariki utakaofanyika Kiomboi mjini, mji ambao ni makao makuu ya wilaya hiyo iliyopo katika jimbo linaloshikiliwa na mbunge Mwigulu Nchemba na baadaye kumaliza siku hiyo kwa mkutano utakaofanyika Manispaa ya Singida (Singida mjini).
Yahaya alisema Jumapili Dk. Slaa atafanya mkutano makao makuu ya tarafa ya Sepuka eneo linaloshikiliwa na mbunge mkongwe nchini, Mohamed Misanga, kabla ya kumaliza ziara yake mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment