Tuesday, August 13, 2013

Hali tete CCM Bukoba

 HONGO YATEMBEZWA, MADIWANI WATISHWA KUNG’OLEWA
HATUA ya madiwani wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika manispaa ya Bukoba, kusaini hati ya tuhuma na kuiwasilisha barua hiyo kwa mkurugenzi wa manispaa hiyo, kumtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kutokuwa na imani na meya anayetuhumiwa kujiingiza katika miradi ya kifisadi imechukua sura mpya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana jioni kutoka mjini Bukoba, zilisema kuwa msimamo huo umewagawa viongozi wa CCM mkoa wa Kagara na hivyo kuitisha kikao cha halmashauri ya mkoa leo kwa ajili ya kuwajadili na kuwafukuza madiwani hao.
Hata hivyo uamuzi huo, huenda ukakigharimu chama hicho kutokana na madiwani hao kusisitiza msimamo wao, wakisema wako tayari kufukuzwa kwa sababu wanatetea maslahi ya wananchi wakipinga ufisadi.
Akizungumza kwa simu na gazeti hili kwa masharti ya kuhifadhiwa jina lake, mmoja wa madiwani hao alisema kuwa rushwa imekuwa ikitembezwa waziwazi kwa wajumbe wa vikao mbalimbali vya CCM ili kuwalazimisha wakutane mara kwa mara kufikia uamuzi huo.
Chanzo hicho kimedokeza kuwa katika kuwagawa madiwani hao ambao wameungana na wenzao wa vyama vya CHADEMA na CCM ili kupunguza idadi ya akidi, diwani mmoja alijaribiwa kuhongwa milioni 20 ili aondoe jina lake katika orodha hiyo.
“Mwenzetu mmoja kwa kweli amekuwa jasiri wa ajabu, juzi aliitwa mahala akatumiwa watu wakiwa na fedha taslimu milioni 20 lakini alikwepa mtego huo na kuwakimbia watu waliotumwa, akisisitiza kuwa hawezi kutusaliti. Sasa kwa hali hii kama CCM wanadhani wanaweza kukinusuru chama kwa kutufukuza na wajaribu waone,” alisema.
Naye diwani mwingine alidokeza kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wilaya na mkoa ndio wanatumika kuwarubuni madiwani hao kwa rushwa ili waondoe tuhuma hizo dhidi ya meya, Anatory Amani.
Hivi karibuni, madiwani hao walimgeuka Rais Jakaya Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao.
Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba, Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.
Walisema Rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Barua ya madiwani hao, iliwasilishwa jana asubuhi saa 2.30 na kupokelewa na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shimwela L.E, ikiwa na saini za madiwani 16 kati ya 24 waliopo.
Hata hivyo, mkurugenzi huyo, alipotafutwa na gazeti hili alishindwa kukiri au kukanusha kupokea barua hiyo, akisingizia kuwa kwa muda huo alikuwa akitekeleza majukumu yake nje ya ofisi.
“Unajua Rais juzi aliacha maagizo mengi na baya zaidi ni lile la ugawaji wa viwanja, hivyo asubuhi niliingia ofisini na kutoka kuelekea mitaani. Nitakupa taarifa kesho kama barua hiyo imefika,” alisema.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Kanuni hizo pia zinaelekeza kuwa mkugenzi atapaswa kuitisha kikao hicho ndani ya siku saba kuanzia tarehe aliyopokea barua ya tuhuma hizo za madiwani na ndani ya muda huo anapaswa kuwa amempatia mtuhumiwa tuhuma hizo ili aweze kuzijibu.
Alisema walikuwa wamesaini madiwani 16 lakini waliamua kumtoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali, hivyo walibakia madiwani 15. Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono itakapofika hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.
Madiwan hao wanaompinga meya ni Richard Gaspar (CCM), Rabia Badru (CUF), Murungi Kichwabuta (CCM), Winfrida Mukono (CHADEMA), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (CCM), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Deusdedit Mutakyahwa (CCM), Robert Katunzi (CCM), Samwel Ruhangisa (CCM) na Dauda Kalumuna (CCM).
Wengine ni Dismas Rutagwelela, Israel Mlaki wa CHADEMA na Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho pamoja na Ibrahim Mabruk, Felician Bigambo wa CUF.

No comments:

Post a Comment