Tuesday, August 13, 2013

CHADEMA yaitikisa CCM uchaguzi Kwembe

KUMEIBUKA ushindani wa vuta ni kuvute kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kinyang’anyiro cha uchaguzi mdogo wa uenyekiti wa mtaa wa Luguruni, kata ya Kwembe, Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili katika ofisi ya serikali za mtaa huo ulionekana kuwa na dalili za upinzani mkali kutokana na vyama hivyo kila kimoja kutamba kuibuka na ushindi.
Tangu asubuhi vituo vya kupigia kura vilionekana na makundi ya watu mbalimbali na kadiri muda ulivyozidi kwenda idadi ya makundi hayo iliongezeka.
Hali hiyo ilisababisa baadhi ya wakazi wa mtaa huo kulalamika kuwa kuna baadhi ya watu ambao si wakazi wa mtaa huo wamekwenda kupiga kura.
Katika uchaguzi huo uliotawaliwa na vituko vya kila aina, kura zilipoanza kuhesabiwa, baadhi ya wafuasi wa CCM wakianza kuimba na kushangilia ushindi kabla ya matokeo kutangazwa huku wengine wakivua nguo hadharani.
hali hiyo ilisababisha ulinzi kuimarishwa kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi unamalizika kwa amani na ilipofika majira ya saa 1:45 usiku matokeo yalitangazwa huku mgombea wa CCM, Saidi Mahandula akiibuka mshindi baada ya kupata kura 286 dhidi ya 206 za mpinzani wake, Mukoba Mukoba wa CHADEMA.
Wakizungumza baada ya matokeo hayo kutangazwa, baadhi ya wananchi walisema uchaguzi huo haukuwa wa haki kwani watu waliopiga kura si wakazi wa mtaa husika.
Uchaguzi huo umefanyika baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Gilbert Mpanduli (CCM), kujiuzulu tangu mwaka 2010 kutokana na kuwapo kwa mgogoro wa ardhi kati yake yeye na madiwani wa Kwembe.

No comments:

Post a Comment