Wednesday, July 10, 2013

VICENT NYERERE: Nilivutiwa na uadilifu wa CHADEMA

MWAKA 2005 ulifanyika uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani ukivihusisha vyama vingi vya siasa, ambavyo vimesajiliwa kwa mjibu wa sheria.
Katika uchaguzi huo, Watanzania wengi kuptia vyama vyao vya siasa walijitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika maeneo yao.
Mmoja wa watu waliojitokeza kuwania nafasi ya uongozi, kwa ngazi ya ubunge, alikuwa Vicent Nyerere, kijana anayetokea katika familia ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa taifa hili na mwanzilishi wa chama cha TANU ambacho kilikuja kuzaa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Vicent hakuwa wa kwanza kuwashangaza Watanzania wengi ambao hawakutegemea wanafamilia ya Nyerere wathubutu kukipa mgongo chama kile alichokiasisi mzazi wao.
Itakumbukwa kwamba mwanafamilia wa kwanza kupingana na msimamo wa baba yake kiitikadi, alikuwa mtoto wa Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere.
Huyu alipingana na baba yake katika majukwaa wakati ule wa mwaka 1995, alipoachana na CCM na kujiunga na Chama cha NCCR-Mageuzi, kilichotikisa nchi, chini ya uongozi wa aliyepata kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Lyatonga Mrema.
Taifa bado linakumbuka namna Makongoro alivyowachachafya CCM kwa hoja nzito, akiwashawishi wananchi wasikubali kukipa tena mamlaka ya kuongoza nchi, kwa sababu nyingi za msingi.
Makongoro akawa kivutio kikubwa, hasa pale alipotoa hoja nzito, akiwahoji Watanzania ikiwa yeye mwenyewe aliyekulia Ikulu, akala mapochopocho ya kuwa mwana wa rais amekipa kisogo chama cha baba yake, inakuwaje mlala hoi wa kijijini asiyejua hata chai ya maziwa ikoje; asiyejua hatima ya maisha yake akiugua; asiyejua kama kesho atakula nini, aendelee kuikumbatia CCM?
Sio siri kwamba Charles Makongoro Nyerere, aligusa mioyo ya wengi na ndiyo maana haikuwa ajabu aliposhinda kwa kishindo kiti cha ubunge akitokea Mkoa wa Arusha.
Hata hivyo, hayo ya Makongoro yamebaki historia kwa sababu, hatimaye alirejea CCM na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani Mara kabla ya kuangushwa hivi karibuni na kijana mwingine.
Kutokana na historia hiyo, wengi walijua kusingeibuka mwana ukoo mwingine wa Nyerere kufanya kama kile alichokifanya Makongoro. Walikosea!
Uchaguzi Mkuu uliopita, umemwibua kutoka mafichoni, mtoto mwingine wa familia ya Nyerere; Vicent Nyerere. Huyu ambaye sasa ni Mbunge wa Musoma Mjini, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Nilipopata bahati ya kuzungumza naye, katika makala ya mwanasiasa wa wiki, swali langu la kwanza kwake lilikuwa kwanini hakuwania ubunge kupitia CCCM ambayo baba yake mkubwa alikuwa mwasisi wake.
Bila kutafuna maneno, akiwa kama vile alijua ningeanza na swali hilo, Vicent kwa kujiamini alisema hakuwa tayari kujiunga na CCM kutokana na chama hicho kukumbatia rushwa, ufisadi na kufanya matendo ya dhuluma kwa wananchi.
Anasema hakuona haja ya kubaki katika chama ambacho ingekuwa kazi bure kukirekebisha akiwa ndani, kutokana na kile alichosema kuoza kimaadili kwa viongozi wengi tangu ngazi ya juu hadi chini.
“CCM ina wenyewe na kwangu mimi isingekuwa rahisi kuwa ndani ya CCM na kuthubutu kuirekebisha. Huwezi kutengeneza nyumba ukiwa ndani, lazima uhame kwanza ndipo uifanyie marekebisho na mimi niliona mahali salama pa kuhamia ni CHADEMA.
“Lakini kikubwa zaidi kilichonichukiza ni kuona yale mema mengi aliyoyaacha mwalimu hayakuendelezwa na badala yake yaliharibiwa yote,” anasema na kutolea mfano wa kuuzwa na kutelekezwa kwa viwanda, mashirika na makampuni mengi ya umma ambayo yalikuwa yakifanya kazi vizuri.
“Lakini baada ya kuona Mwalimu amestaafu uongozi, hawa ndugu zetu wa ‘magamba’ waliyatafuna yote na leo kilichobaki sasa ni aibu. Ningewezaje kwa mtu makini yeyote yule kwenda kuungana na watu wasioitakia mema nchi hii na waliouza rasilimali zetu na kujinufaisha wao wenyewe na watoto wao,” anaongeza.
Vicent anasema alichukua uamuzi wa busara licha ya kulaumiwa na kushutumiwa na baadhi ya watu wakiwemo wale wa CCM wa kujikomboa kutoka katika makucha ya mafisadi na kujiunga na CHADEMA, alichokiita kimejaa viongozi na watu wenye maono ya mbali na ambacho sera zake zina uchungu na nchi. Ana imani kubwa na CHADEMA kiasi kwamba msimamo wake hauwezi kuyumba kamwe.
Anasema CHADEMA ni chama imara na chenye mtazamo wa mbali ukilinganisha na vyama vingine licha ya njama zinazofanywa hivi sasa za kuikosanisha na wananchi ili waione haifai, lakini kwa bahati nzuri njama hizo Watanzania wengi wameshazifahamu.
“Watanzania wenyewe wanaona kazi zinazofanyika na CHADEMA, kwa mfano nenda kwenye majimbo yote ya CHADEMA kazi zimefanyika, lakini kwa wenzetu kazi kubwa wanayofanya ni kugawana ‘ten pacent’ (asilimia kumi) ingawa wamekuwa mashujaa wa kujisifu. Lakini je, ni kweli wanatenda yale wanayoyasema?
“Kwa mfano kesi nyingi zilizoko mahakamani dhidi ya viongozi wa CHADEMA ni za kubambikizwa na za kutaka kutuzuia tusiseme ukweli ili wananchi wafahamu kinachoendelea katika nchi hii. Kinachofanyika ni kutaka kutugombanisha sisi na Jeshi la Polisi.
“Tunajua wapo watu katika nchi wamepata madaraka kwa njia ya mkato, ambao sasa wanatumia rasilimali za nchi kwa fujo na kwa manufaa yao. Na hao ndio wamekuwa wakilitumia vibaya jeshi letu, maana hata polisi wenyewe husema kuwa hawapendi kutupiga mabomu kwenye mikutano yetu bali huamriwa na wakubwa wao,” anasema.
Kuhusu ahadi alizoahidi wakati akiomba kura, mbunge huyo anasema amejitahidi kadiri ya uwezo wake kwa kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya afya, barabara, maji na elimu. Kwamba tofauti ipo kubwa wakati wake na wakati wa mbunge wa CCM.
Anasema lengo lake ni kuhakikisha anatimiza yale aliyowahidi wananchi wa jimbo lake, kwani hataki kusutwa siku atakapotoka kwenye uwakilishi.
“Mimi sitaki kuwa mbunge wa ahadi ambazo hazitekelezeki. Sisi CHADEMA kazi yetu ni kufanya kwa vitendo, na nina imani kubwa na wananchi wa jimbo langu walionichagua kuwawakilisha na ndiyo maana nimekuwa nikipiga kelele sana. Na hii yote ni kutaka kulipa yale niliyoahidi kwa wapiga kura wangu na wala si vinginevyo,” anasema.



Ndoto za urais
Anasemaje kuhusu kuwania nafasi ya urais kama inavyoshuhudiwa katika nchi nyingi za Afrika, ambako baadhi ya watoto wa waliokuwa watawala wa nchi hizo, nao wamepata bahati ya kukalia viti walivyoketi wazazi wao?
“Sina mpango huo hadi nimalize kazi ya jimbo kwanza. Hivyo suala la kugombea urais siwezi kulizungumzia sasa hivi kwani ahadi yangu kwa wananchi wa Jimbo la Musoma bado haijakamilika,” anasema.
Vicent anaeleza kuwa anaamini kwa nafasi yake ya ubunge anaweza kuwatumikia watu kikamilifu na kwa kiwango kitakachosaidia kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, vikundi na hatimaye jimbo kwa ujumla na hivyo kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Kuhusu tabia ya baadhi ya makada wa CCM ambao wameanza kujipitisha katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutaka urais, Vicent anasema wote hao hawana sifa zozote za kumkabili yule atakayependekezwa na CHADEMA.
Anaongeza kwamba hakuna mgombea yeyote iwe wa urais, udiwani, ama ubunge kutoka CCM anayeweza kushindana na yule wa CHADEMA na kushinda, kwa sababu Watanzania wamechoka utawala mbovu wa CCM.
“Hata sasa, CCM haijawahi kushinda kihalali katika chaguzi nyingi. Wanashinda kwa kutoa rushwa, kwa vitisho, kwa kununua watu na kuiba kura.
“Kimechokwa na wananchi kiasi kwamba leo hii wengi wanaogopa hata kuvaa magwanda yao na kutembea nayo barabarani kwa maringo na kujiamini kama ilivyokuwa zamani.
“Na ukitaka kujua CCM ni weupe, hawana tija tena kwa wananchi, tuitishe uchaguzi katika jimbo langu, tufanye kampeni za kistaarabu, na iwepo tume huru, uone aibu ya mwaka watakayoipata,” anasema.

No comments:

Post a Comment