MFUMO wa muungano wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, umepingwa na wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya Kusini na Kaskazini Unguja tangu kuanza kwa mjadala huo Julai 12, mwaka huu.
Msimamo huo umejitokeza baada ya wajumbe wa mabaraza ya katiba kukaa kama kundi la kujadili fungu la muungano katika rasimu ya katiba katika Wilaya ya Kati, Kaskazini ‘A’ na ‘B’, ambapo wajumbe wanaotetea mfumo wa serikali mbili waliendelea kutamba katika mabaraza hayo.
Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Awadh Ali Said, alisema kwamba tangu tume hiyo kuanza kazi Mkoa wa Kaskazini na kufanya kazi katika wilaya tatu, wananchi wanaotaka mfumo wa muungano wa serikali mbili wameonekana kuwa ni wengi tangu tume hiyo kuanza kazi visiwani Zanzibar.
“Miundo ya muungano inayozungumzwa kwa upana ni miwili tu, hasa muungano wa serikali mbili na tatu kama ilivyopendekezwa na tume, maoni ya muungano wa mkataba nafikiri yamebadilika, hoja zilizobaki ni serikali mbili na tatu,” alisema Awadh.
Alisema wananchi wameonyesha uelewa mkubwa wa kile walichokuwa wakijadili na kuweza kuipitia rasimu ya katiba kifungu kwa kifungu na kutoa michango mizito ambayo itaisaidia sana tume kupata katiba mpya lakini aliongeza kusema kuwa katiba itatokana na maoni ya wananchi, mabaraza ya katiba na bunge la katiba kabla ya wananchi kupiga kura na kuamua.
Kamishina huyo alisema ni jambo la faraja kuona wananchi wamekuwa watulivu na kuzungumza kile wanachokiamini na tume imewataka wananchi kuendelea na utulivu, kujenga uvumilivu na kuheshimu hoja ya mwingine hata kama itatokea tofauti ya kifikra na kimtazamo.Wakijadili rasimu hiyo ndani ya ukumbi wajumbe hao, Abdallah Kombo Baraka, alisema mfumo uliopendekezwa wa serikali tatu ni kinyume cha makubaliano ya mkataba wa Tanganyika na Zanzibar uliosainiwa na waasisi wa Muungano huo, Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
Akifafanua huku ukumbi ukibaki kimya, alisema makubaliano ya waasisi kwa niaba ya nchi zao ni kuwapo kwa muungano wa serikali mbili na kwamba makubaliano hayo yamewasilishwa Umoja wa Mataifa na kutambuliwa.
“Serikali tatu ni kuunda taifa jingine, wakati lengo la mabadiliko ni kurekebisha Katiba na si kuvunja muungano au kuunda taifa jipya ndani ya taifa lililopo,” alisema Baraka na kuongeza kuwa kifungu cha 57(1) kifutwe katika mapendekezo hayo.
Mohamed Silima Chum, alisema katika umri wa maisha yake aliona mengi na kuupinga mfumo wa serikali tatu kuwa utalivuruga taifa na hatimaye kuyapa majeshi nafasi ya kunyakua dola kila wakati au kufanyika kwa mapinduzi ya kijeshi mara kwa mara.
Alisema Watanzania wajifundishe umuhimu wa uzalendo na utulivu wa kitaifa kwa kuangalia yanayochomoza katika mataifa ya Misri, Syria, Sudan na kukatika kwa taifa la Ethiopia na Eritrea.
Mjumbe Furaha Khamis Mshenga alisema suala la serikali tatu linagubikwa na utata na kwamba linaweza kuibua mzozo utakaoliyumbisha taifa na kulisambaratisha.
Mshenga alisema ikiwa Rais wa Tanganyika atatoka chama ‘A’, Rais wa Zanzibar chama ‘B’ na wa Muungano chama ‘C’, utakuwa ni mtikisiko, pia utii wa vyombo vya ulinzi na usalama utalegalega na kukosa ustawi.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha kazi yake katika Mkoa wa Kaskazini Unguja na Julai 25 itaanza kukusanya maoni katika Wilaya ya Mjini, huku suala la muungano wa mkataba likionekana kupwaya na kukosa mashiko kwa wananchi, tofauti na ilivyokuwa ikipigiwa debe na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Wajumbe wa mabaraza ya katiba katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ walisema rasimu ya Katiba mpya imejaa upungufu na kutoa mfano wa utangulizi wa katiba hiyo ulioahidi kuenzi misingi ya muuugano iliyowekwa na waasisi wakati ibara ya 57(1) ikipendekeza kuubomoa muundo wa muungano wa serikali mbili ulioasisiwa na Rais Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.
wazanzibari hatukubali mfumo wa muungano uliopo sasa.Rasimu ya katiba ilikusanya mawazo ya wananchi waliowengi na kuona kuna haja ya kuwepo kwa mfumo wa muungano wa serikali tatu ambazo ndio muarubaini pekee wa kutatua kero zilizokuwepo kwa muda mrefu ambapo hadi sasa hakuna dalili yoyete ya kuondoka.Wanzanzibari tunachotaka ni mamlaka kamili ya nchi yetu tuweze kujiamulia mambo tutakayoona ndio tija kwa taifa letu.Ieleweke kinyume na maoni yaliowengi katika mpya haitopigiwa kura ya maoni na hivyo kupelekea Zanziba kujitenga.
ReplyDelete