MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimpatia ruhusa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky, ya kwenda nje ya nchi kutibiwa.
Sambamba na hilo, Hakimu Mkazi Alocye Katemana, ametoa onyo kwa mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Ludovick Joseph, asiendelee kuiongelea kesi hiyo nje ya mahakama kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Mahakama hiyo imesema endapo atakaidi onyo hilo haitosita kumfutia dhamana yake.
Wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere, aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba wanaiomba mahakama impatie ruhusu mteja wake aende nje ya nchi kutibiwa kwani anasumbuliwa na matatizo ya mgongo.
Wakili huyo alitoa nyaraka za matibabu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo inaonyesha Lwakatare ni mgonjwa na anahitajika kutibiwa nje ya nchi.
Kicheree pia aliulaumu upande wa jamhuri kwa kukaa kimya bila kulalamika wakati kesi ambayo bado haijaisha mahakamani kuandikwa magazetini, akimtuhumu Ludovick kushiriki jambo hilo.
Baada ya kuwasilisha madai hayo, mahakama ilitoa kibali cha Lwakatare kwenda kutibiwa nje, ambapo leo (jana) hakuwepo mahakamani na pia ilitoa onyo kwa Ludovick. Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 21 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Machi 18 mwaka huu, ilidaiwa na upande wa jamhuri kuwa Lwakatare na Ludovick wanakabiliwa na kosa moja la kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.
No comments:
Post a Comment