Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeng’ang’ania msimamo wake wa kutomtambua Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa, hadi pale atakapoachia madaraka katika ofisi hiyo.
Katibu mkuu wa Chama hicho, Dk.Willbroad Slaa, alitoa msimamo huo ,muda mfupi baada ya kufungua mkutano wa kimataifa wa Bodi ya Vijana wa Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia Duniani (IYDU) jijini Dar es Salaam.
Alisema Tendwa amekiuka maadili ya uongozi wa kazi yake wa kuwa mlezi wa vyama vya siasa hapa nchini badala yake amekuwa mlezi wa chama kimoja ambacho ni Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Sisi tumemfuta katika listi yetu, na ndiyo maana katika mawasiliano ya barua hatumuandikii barua yeye bali inasainiwa na watu wengine katika ofisi hiyo,” alisema Slaa.
Aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo hawajavunja sheria yoyote kwa kuwa wamefuata sheria na taratibu zote, na kueleza kuwa Chadema wanaiheshimu ofisi ya msajili wa vyama vya siasa lakini siyo msajili wa vyama vya siasa.
Alisema sababu za kutomtambua Tendwa, zimetokana na yeye mwenyewe kutokuwa makini katika suala la malezi ya vyama vya siasa na badala yake anatumika kama msemaji wa chama kimoja ambacho ni (CCM).
“Huyu mtu sio mlezi wa vyama kama alivyoainishwa, kwa sababu hatutambui Chadema, na sisi tunaiheshimu tu ofisi ya msajili, kwa sababu tunahisi anatumiwa kwa maslahi ya kundi fulani,” alisema bila kufafanua aina ya kundi.
Dk. Slaa aliongeza kuwa kutokana na taswira hiyo inaonyesha dhahiri kuwa, Tendwa anafanya vitu kwa hisia huku akiwa hana sheria hata moja anayoisimamia.
Alisema Chadema kinashangazwa na hatua ya baadhi ya vyombo vya dola kutumika kama chombo cha siasa cha kuwanyanyasa, kuwanyima vijana uhuru wa kuchagua aina ya chama kwa sababu vimewajenga hofu kutokana na adha wanayokumbana nayo.
“Chama kitaendelea kuweka wazi mambo yote yanayofanywa na vyombo vya dola ili mradi tu kifuate sheria zake, hasa yale yanayowagandamiza wananchi kwa sababu yanaharibu demokrasia ya nchi,” alisema Dk. Slaa.
Aliitaka serikali kutojadili suala la uvunjifu wa amani kwa sababu imesababisha yenyewe, kwa kushindwa kuwadhibiti baadhi ya viongozi wake wenye uchu na rasilimali za nchi.
Slaa alisema muda wa Tendwa kuwa madarakani umeisha siku nyingi lakini mpaka leo bado yupo, hivyo inadhihirisha kuwa amewekwa na watu fulani kusaidia chama tawala.
Kuhusiana na tuhuma za Chadema kuanzisha kikundi cha Red Brigade, Slaa alisema hilo siyo jambo la kushangaza kwa kuwa ni kikundi cha ulinzi kama vilivyo vikundi vingine vinavyolinda katika nyumba na ofisi.
Alisema Red Brigade ilianzishwa mwaka 2004 na Chadema walimpelekea msajili vipengele vyote muhimu vilivyomo katika katiba, lakini msajili alijibu kwa lugha ya ukali huku akituhumu kukifuta chama hicho.
Alisema Januari 2005, Chadema ilimjibu msajili kwa maelezo nia na dhumuni ya kuanzishwa kwa kikundi hicho , lakini msajili huyo alishindwa kuwathibitishia Chadema ni kifungu gani kinachokataza kuanzishwa kwa kikundi hicho.
Mkutano huo wa IYDU unafanyika jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha wajumbe wapatao 16 kutoka nchi mbalimbali duniani, utafanyika kwa siku tano, huku Baraza la Vijana (Bavicha) wakiwa wenyeji wa mkutano huo.
Naye Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema katika mkutano huo, mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwamo mauaji yanayofanyika hapa nchini hususani yaliyotokea mjini Arusha, na yeye kuwa mwasilishaji mkuu.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa mkutano huo, Aris Kalafatis, alisema wamekutana nchini kwa ajili ya kuangalia changamoto zinazokikabili Chadema na kuzitafutia ufumbuazi.
Vijana wawakilishi wa nchi hizo ni kutoka nchi ya Kenya, Uganda, Mozambique, Namibia, Togo, Pemba, Italia, Tailand na Austaria.
Hivi karibuni, Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, ilikitaka Chadema kusitisha kambi za mafunzo ya kulinda amani maarufu kwa jina la mgambo, la sivyo itakifuta kwenye usajili wake.
Alisema endapo chama hicho kitakiuka sheria za vyama kitachukuliwa hatua, ikiwemo kukifuta chama.
No comments:
Post a Comment