Katibu Mkuu wa Chadema,Dk Willibrod Slaa amesema Tanzania haiwezi kuendelea kuwa na amani kama wizi wa rasilimali za taifa utaendelea.
Dk Slaa aliyasema hayo Dar es Salaam jana, wakati alipofungua mkutano wa Bodi ya Kimataifa ya Shirikisho la Vyama vya Kidemokrasia kwa Vijana (IYDU) ambao unafanyika kwa mara ya kwanza katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Amani inakuwapo mahali penye haki” alisema Dk Slaa na kutolea mfano wa askari ambao wamekuwa wakikamatwa na nyara za taifa wakati wao ni vyombo vya dola, huku pia akisema migogoro ya ardhi inayokithiri inaweka rehani amani ya taifa hili.
Haki nyingine alizolalamilia Dk Slaa ni pamoja na kuminywa kwa demokrasia ambapo ametolea mfano wa polisi kuzuia mikutano ya Chadema huku akiwatuhumu kuwa wamekuwa mashabiki wa siasa badala ya kutimiza wajibu wa kulinda amani kwenye mikutano hiyo.
Kuhusu msajili wa vyama vya siasa John Tendwa, Dk Slaa alisema Chadema walishamfuta kwenye orodha ya watu wanaowasiliana nao.
Akizungumzia mpango wa chama hicho kuanzisha kikosi cha ulinzi, Katibu huyo alisema hata kwenye majumba ya kawaida watu wanakuwa na walinzi wao iweje wao kama chama wasifanye hivyo.
“Kuna walinzi wengi tu wanalinda majumba ya watu mjini, ni sheria gani inayotukataza sisi?” alihoji Dk Slaa.
Kwa upande wa ajira alisema, hakuna nchi inayoweza kuwa na uchumi imara kama vijana wake hawana ajira. Naye Mwenyekiti wa IYDU, Aris Kalafatis alisema ujumbe wao mkubwa kwa vijana wa Tanzania ni kutaka mabadiliko hususan katika masuala ya maendeleo,huduma za jamii na ukosefu wa ajira.
Akizungumzia migogoro mingine inayotokea katika mataifa kama Misri na Tunisia, Kalafatis alisema hawaungi mkono kudai haki kwa njia za machafuko, wanachohitaji ni kuona migogoro inatatuliwa kwa njia za mazungumzo na siyo kama hali ilivyo sasa.
No comments:
Post a Comment