Friday, July 12, 2013

Ni CHADEMA au CCM?

HOFU kubwa ya kutokea tena kwa vurugu katika uchaguzi mdogo wa madiwani kwenye kata nne imeugubika mji wa Arusha na vitongoji vyake.
Hofu hiyo inatokana na ugumu wa uchaguzi huo pamoja na mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita mkoani humo katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani kwa CHADEMA na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 70.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa uchaguzi huo utakuwa na mvutano mkubwa kwa vyama vya CHADEMA na CCM ambavyo idadi ya madiwani wao inakaribiana sana, na ndio utakaoamua nani ataiongoza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, CCM ilikuwa na madiwani 10 wa kata, viti maalumu watatu na wabunge watatu na jumla yao kuwa 16.
CHADEMA nao walipata madiwani wanane wa kata, viti maalumu watatu na wabunge watatu, jumla 14, huku TLP wakiwa na madiwani wawili.
Baada ya matokeo hayo, ulifanyika uchaguzi wa meya na naibu wake, ambao ulitawaliwa na vurugu kubwa, huku CHADEMA wakikataa kumtambua Meya Gaudence Lyimo (CCM).
CHADEMA waliamua kufanya maandamano ya kupinga mchakato uliomuwezesha meya huyo kuingia madarakani na kuzuka vurugu zilizosababisha polisi kuwaua kwa risasi watu watatu.
Tangu wakati huo hadi sasa, mji wa Arusha na viunga vyake haujapata utulivu wa kisiasa, huku CCM ikidaiwa kuendesha harakati za kuidhoofisha CHADEMA na Mbunge wake, Godbless Lema, anayeonekana kuwa mwiba mkali.
Hata hivyo, CCM ilipata ahueni mwaka 2011 pale CHADEMA ilipoamua kuwafukuza uanachama madiwani wake watano kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.
Madiwani wanne walikuwa wa kata na mmoja wa viti maalumu. Madiwani hao ni Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah, Diwani wa Elirai, John Bayo, Diwani wa Themi, Ruben Ngowi, Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed.
CCM nayo ilipata pigo mwaka jana baada ya diwani wake wa Daraja Mbili kufariki dunia, huku diwani wa Sombetini, Alphone Mawazo, akiamua kujiunga na CHADEMA, na hadi sasa kata yake haijatangazwa kuwa wazi kwa sababu ambazo hazijawekwa wazi.



Kinachogembewa
CHADEMA na CCM ugomvi wao mkubwa kwa Jiji la Arusha ni kuongoza halmashauri hiyo na kutoa meya, hivyo uchaguzi wa keshokutwa ndio utaamua majaliwa ya nafasi ya meya aliyepo hivi sasa anayetoka chama tawala.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa mgumu zaidi kwa pande zote mbili kutokana na kupungua kwa idadi ya madiwani, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2010.
Safari hii CCM ina madiwani wanane wa kata, madiwani wa Viti Maalumu watatu na wabunge watatu ambapo jumla yao ni 14.
CHADEMA wenyewe wana madiwani watano wa kata, viti maalumu watatu na wabunge watatu, ambapo jumla yao ni 11.
Kama CHADEMA itafanikiwa kurejesha kata zake nne, itakuwa na madiwani wa kata tisa, wabunge watatu na madiwani wa viti maalumu watatu, hivyo kufanya idadi yao kuwa 15, hivyo kuwazidi CCM kwa diwani mmoja.
Idadi hiyo itawafanya wawe na uwezo wa kuongoza halmashauri hiyo na kutoa meya wa jiji hilo, kwani wakiingia kwenye baraza la madiwani wanaweza kumng’oa wa CCM na kumchagua wa kutoka chama chao.
CCM wanaweza kulingana na CHADEMA kama watafanikiwa kumshawishi Diwani wa TLP, Michael Kivuyo, kuwaunga mkono kwenye kura za umeya, hivyo pande hizo kila moja kuwa na madiwani 15.
Kama hali itakuwa hivyo, pande hizo mbili zitalazimika kukaa kwenye meza ya mazungumzo kukubaliana utaratibu wa kuongoza halmashauri ya jiji kwa kupokezana kwa kipindi fulani.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima kuwa uchaguzi wa kesho kutwa utakuwa mgumu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea huko nyuma.
Tayari kuna taarifa kuwa idadi kubwa ya viongozi wa CCM wamepiga kambi mkoani humo kuhakikisha wanapata walau kata moja au mbili ili kuendelea kuiongoza halmashauri ya jiji hilo ambalo ni kivutio kikubwa cha utalii.
Ugumu wa uchaguzi huo
Ugumu wa uchaguzi huo pia unachangiwa na mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita kwenye mkutano wa kufunga kampeni wa CHADEMA, ambapo watu wanne walifariki dunia na 70 kujeruhiwa.
Baadhi ya watu waliozungumza na Tanzania Daima walionesha wasiwasi wao juu ya usalama siku ya uchaguzi huku wengine wakieleza kuwa wanahofia kujitokeza siku ya kupiga kura.
Simon John, mkazi wa Kata ya Themi alisema bado ana hofu ya kujirudia kwa matukio ya kupigwa mabomu kama yalivyojitokeza awali.
Joyce Tumaini, mkazi wa Kimandolu alisema mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita unaweza ukasababisha watu wachache kujitokeza kupiga kura.
Usalama safi
Mkurugezi wa Jiji la Arusha, Sipora Liana, amewataka wakazi wa jiji hilo kujitokeza kwa wingi kuhitimisha uchaguzi mdogo wa kata nne zilizosalia baada ya uchaguzi huo kuahirishwa awali kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea Juni 16 na kuua watu wanne na wengine 70 kujeruhiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, Liana alisema hali ya usalama imeimarishwa na hakuna hofu ya kutokea milipuko katika uchaguzi huo aliosema utaanza saa 1 asubuhi hadi saa 10 jioni.
Alitaja kata zitakazochagua madiwani wao kuwa ni Kaloleni, Themi, Kimandolu na Elerai, huku akiainisha kuwa vituo katika kata zote ni 136 na kila kituo kitakuwa na msimamizi mmoja.
Aliongeza kuwa wapiga kura waliojiandikisha ni 60,123 na kwamba wamekubaliana na viongozi wa vyama vya siasa mkoani humo kuwataka wafuasi wao kuondsoka katika maeneo ya kupigia kura baada ya zoezi hilo kukamilika kwa kila mmoja.

No comments:

Post a Comment