Thursday, July 11, 2013

Mbowe alishutumu JWTZ, Polisi kutesa raia Mtwara

Wenyewe wamjibu kwamba hizo ni siasa
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imesema matukio ya ubabe, unyanyasaji, uonevu na matesi ya siri yanayoendelea mkoani Mtwara ni ishara ya serikali kushindwa kutafuta suluhisho la sakata hilo kwa njia ya amani.

Hayo yalisemwa  na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi ya kikao cha Kamati Kuu ya chama kilichofanyika Julai 06 na 07, mwaka huu.

Kikao hicho kilijadili hali ya kisiasa nchini na rasimu ya Katiba.

Alisema kwa haraka hali ya Mtwara inaonekana ni shwari lakini kuna vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa na Polisi na wanajeshi kwa kutumia silaha kuwakamata wananchi na viongozi wa kisiasa na kuwapeleka kwenye kambi za jeshi kwa lengo la kuwatesa.

“Rais Jakaya Kikwete alitangazie Taifa ‘hali ya hatari’ kwa mkoa wa Mtwara, kama anaona ni hatari kiasi cha kutumia Jeshi la Wananchi (JWTZ), kuzunguka mitaani na silaha za kijeshi, ili Taifa liweze kujua,” alisema.

Aidha, alisema CC imesema kama Jeshi la Polisi limeshindwa kutekeleza majikumu yake kwa mujibu wa sheria atangaze kulivunja jeshi hilo mara moja.

Mwenyekiti huyo alisema pia serikali iunde Tume Huru ya kuchunguza matukio ya mauaji, ubakaji, utesaji na ukiukwaji wa Haki za Binadamu yanayofanywa na vyombo vya dola na waathirika wote waweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria.

Sakata la gesi Mtwara, lilianza Novemba 16, mwaka huu, baada ya serikali kutangaza mpango wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mkoani humo hadi Dar es Salaam, na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, kutangaza Bungeni msimamo wa serikali wa kuendelea na ujenzi wa bomba hilo.

Watu wanne wamefariki na wengine 15 wamejeruhiwa kwa risasi na 15 majeraha yaliyotokana na kurupushani za kujiokoa dhidi ya vurugu za mwezi Mei, mwaka huu.

JWTZ WAMJIBU MBOWE

NIPASHE ilipomtafuta msemaji wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) Kanali Kapambala Mgawe,  kuzungumzia tuhuma hizo, alisema hazina ukweli wowote na hataki kuendelea kuzungumzia suala la Mtwara kwa sababu limekaa katika mlengo wa kisiasa.

“Jeshi la Wananchi lina nia njema ya kuhakikisha amani inalindwa kwa wananchi wote wakiwamo wa Mtwara na si vinginevyo, hakuna ukweli wowote kwamba Wanajeshi wanawatesa wananchi wa Mtwara,” alisema na kuongeza:

“Nimefika mahali nimechoka kuzungumzia suala la  Mtwara,  suala hili naliona liko katika mlengo wa kisiasa zaidi wakati mimi siyo mwanasiasa na sitaki kugombana na wanasiasa…sipendi tabia ya watu kutufanya kama vile hatujui tunachokifanya, tunataka amani ilindwe na shughuli za kuendeleza uchumi wetu zifanyike salama,” alisema.

NIPASHE pia ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Advera Senso, kuzungumzia juu ya mkakati wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuendesha makambi ya mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wake kulinda Viongozi wao, alisema ni marufuku kufanya hivyo na wakithubutu watachukuliwa hatua za kisheria

No comments:

Post a Comment