Kuanzia Julai 12 hadi Agosti 2, mwaka huu, kutakuwa na mikutano ya Mabaraza ya Katiba ambayo yatoa ushiriki mpana kwa kila mjumbe kuchangia na kutoa mawazo yake kwa uhuru na uwazi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, mikutano hiyo ni ya kujadili na kutoa hoja za msingi kwa maslahi ya Taifa na si kupiga kura au kutetea maslahi ya kundi au watu fulani.
Jaji Mstaafu Warioba anasema wajumbe wa mabaraza hayo watashiriki kutoa mawazo yao kwa uhuru bila kuingiliwa na taasisi au mtu yeyote ili kupata Katiba yenye maslahi ya taifa.
Wajumbe wa Mabaraza takribani 20,000 wamepata Rasimu hiyo ya Katiba pamoja na mashirika, ambapo Tume hiyo imepanga kuanzia Julai 12, mwaka huu itaanza kugawa Rasimu hiyo katika kila kijiji ili kuifikia nchi nzima.
Tume itatumia siku 54 katika kuendesha Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa nchi nzima na imejigawa katika makundi 14 na kila kundi litaendesha mikutano hiyo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 12 au 13.
Wakati mabaraza haya yakijiandaa kuanza kukutana kuanzia Ijumaa ijayo kufanyakazi hiyo adhimu, tunapenda kuwakumbusha wajumbe wa mabaraza hayo kutimiza wajibu wao mkuu kwa uhuru na kwa maslahi ya taifa na si kuangalia utashi binafsi au makundi fulani fulani katika jamii.
Ni vizuri kila mjumbe akashiriki kutoa maoni bila ya kuingiliwa na mtu yeyote kwa kuzingatia taratibu ambazo zimewekwa na Tume katika kuendesha na kusimamia mikutano hiyo.
Tunasema hivyo, kwa kuwa kumeanza kujionyesha viashiria vya baadhi ya watu au makundi vikiwamo vyama vya siasa, kutaka kuhodhi mjadala huu muhimu ambao utatoa mustakabali wa taifa letu kwa miaka mingi ijayo.
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba wanatakiwa kuwa makini sana katika kuchambua rasimu iliyotolewa na Tume ya Katiba kwa kutambua kuwa mzaha wowote watakaoufanya au kuingiza ushabiki wowote usio na siha njema kwa taifa, kunaweza kuleta athari kubwa au mgawanyo miongoni mwa wananchi na matokeo yake ni kuvunjavunja misingi ya amani na mshikamano tuliyoachiwa na waasisi wa Taifa hili.
Wajumbe wahakikishe wanaepuka kutekwa na mijadala inayojikita katika masuala ya siasa, utawala na muungano pekee kama inayoonekana hivi sasa katika mijadala mbalimbali miongoni mwa wananchi, wasomi na wanasiasa.
Bali pia wanapaswa kuhakikisha wananajikita katika kuchambua kwa umakini mkubwa masuala mengine makubwa na muhimu kama vile haki za raia na binadamu, masuala ya ardhi, jinsia, walemavu, haki za watoto na wanawake na makundi mengine yaliyosahaulika katika jamii.
Tunatoa shime kwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kwa umakini mkubwa bila ya kuingiliwa na misuguano ya kisiasa, bali kuzingatia maslahi mapana ya Taifa ili Katiba itakayopatikana ipafanye Tanzania kuwa mahali pazuri na salama kuishi kwa kila mmoja wetu.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mhariri Nipashe
No comments:
Post a Comment