Friday, July 19, 2013

‘Hatuna haja na meya wa Arusha’

SUALA la nafasi ya meya wa jiji la Arusha limechukua sura mpya, baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kudai kuwa sio ajenda yao ya sasa.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Kanda ya Kaskazini wa CHADEMA, Amani Golugwa, alipozungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa kwamba kwa sasa madiwani wa chama hicho wamejipanga kuweka mikakati madhubuti ya kupanga na kusimamia miradi ya maendeleo iliyo kwenye halmashauri hiyo kwa ushirikiano wa karibu na wananchi kwa manufaa ya taifa.
Alisema pamoja na ukweli kuwa taratibu zilizotumika kumweka Meya Gaudence Lyimo madakani hazikuwa sahihi, lakini kwa sasa kipaumbele chao ni kushughulika na maendeleo ya wananchi.
Suala la nafasi ya meya wa jiji hili, lilisababisha maafa makubwa wakati chama hicho kilipopinga kanuni zilizomweka madarakani.
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemtaka Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, kuacha unafiki wa kupinga kodi ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu wakati wabunge wa chama chake ndiyo walioipitisha.
Golugwa alisema kuwa kodi hiyo ilipitishwa kwa kishindo na wabunge wa CCM ambao ni wengi wakati wale wa CHADEMA walipokuwa kwenye maombolezo ya wananchi wanne waliouawa kwa bomu jijini Arusha, hivyo haiwezekani leo CCM kuikataa.
“Tunamsihi Nape aache unafiki; awe mkweli, haiwezekani wabunge wa chama chake wapitishe kodi hii inayowaumiza wananchi hasa wa kipato cha chini halafu yeye akimbilie kwenye vyombo vya habari kuipinga. Kama CCM ilikuwa haikubaliani na kodi hii isingepitishwa bungeni.
Nape anatakiwa aache usanii wa kujifanya hakujua tozo hii ya laini za simu wakati ina baraka ya baraza la mawaziri ambalo linaongozwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, na limepitishwa na wabunge wa chama chake sasa anataka kuwahadaa wananchi kuwa CCM haihusiki,” alihoji Golugwa.
Alisema kuwa tayari CHADEMA imeshaanza mchakato pamoja na wabunge wake ili kuona namna suala hilo litakavyoshughulikiwa ikibidi hata kwa kupeleka hoja binafsi bungeni ili kuhakikisha kodi hiyo inayowaumiza wananchi walio wengi inaondolewa.
Kauli ya Golugwa imekuja siku chache baada ya Nnauye kutoa msimamo wa CCM kuipinga kodi hiyo na kuishauri serikali kuiondoa na itafute njia nyingine ya kuongeza mapato ambapo mamlaka ya mapato nchini (TRA) imesema kwamba itakuwa inakusanya bilioni 28 kwa mwezi kwa kukata sh 1,000 katika kila laini ya simu. Inasemekana kuwa Watanzania wanaotumia simu sasa nchi nzima ni zaidi ya mil. 28.

1 comment:

  1. kwelii kwanza nawapongeza kwa kata nne za arushaa alaf pilli chek hili swala la kodi za simu maana linatuumiza mno!

    ReplyDelete