Friday, July 19, 2013

Baraza lataka Katiba ya Tanganyika

BARAZA la Katiba la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) linatarajia kutoa mapendekezo yake leo ya uundwaji wa Katiba mpya, huku likitaka kusitishwa kwa mchakato huo hadi hapo katiba ya Tanganyika itakapopatikana.
Hilo ni moja ya maazimio yaliyofikiwa jana jijini Dar es Salaam, wakati wa kupitia kipengele kimoja baada ya kingine ndani ya rasimu ya Katiba mpya kulikofanywa na wajumbe wa baraza hilo wapatao 70 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Felix Nielema, mwanaharakati kutoka Wilaya ya Ngara, alisema rasimu hiyo inazungumzia muungano, hivyo kufanya iwe batili, kwani inawalazimisha Watanzania kuingia kwenye muungano bila ya kuwa na katiba yao.
“Jamani katika hili tunatakiwa tuwe makini sana, kwani hawa jamaa tayari wanatulazimisha kuingia kwenye mambo ambayo hatujashirikishwa. Hivyo rasimu hii isimamishwe kwanza, tupate kwanza katiba ya Tanganyika ili tukija kujadili suala la muungano tujue yapi yaingizwe katika muungano na yapi yaachwe,” alisema Nielema.
Wakili Frugence Masawe, alikosoa sura ya 10 ndani ya rasimu hiyo inayoelezea mambo ya mahakama ya muungano wakati ukweli ni kwamba suala la mahakama si la muungano.
Naye Mwangalizi wa Haki za Binadamu kutoka Ukerewe, Benjamin Mtebe, alisema katika kipengele cha uendeshaji wa Bunge, kinaeleza kwamba endapo hoja ya bajeti ya wizara fulani itapingwa na wabunge na kurudishwa kwa ajili ya marekebisho, ikipingwa tena kwa mara ya pili serikali ina uhalali wa kuipitisha hivyo hivyo.
Kutokana utaratibu huu, wajumbe waliokuwa wakijadili kipengele hicho walipendekeza kuwa ni vema bajeti ikarekebishwa hata mara sita mpaka wabunge watakapoiridhia, kwani wao ndio wawakilishi wa wananchi.
Awali Mkurugenzi wa Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia, alisema baraza hilo limepewa kibali halali na Tume ya Kurekebisha Katiba kuichambua rasimu ya Katiba mpya.

No comments:

Post a Comment