Saturday, July 6, 2013

CHADEMA waanza kuichambua rasimu

 KUGUSA PIA MLIPUKO WA BOMU JIJINI ARUSHA
KAMATI Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), inakutana leo kwa siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam katika kikao cha dharura kujadili rasimu ya katiba mpya.
Wakati CHADEMA wakikutana, Tume ya Mabadiliko ya Katiba nayo imetangaza kuanza kuendesha mabaraza ya katiba ya wilaya Julai 12.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene, mbali na rasimu, kikao hicho chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe pia kitajadili masuala mbalimbali.
Alizitaja ajenda hizo kuwa ni taarifa ya hali ya siasa nchini, taarifa juu ya mfumo wa uendeshaji wa chama kwa kanda (uzinduzi) na taarifa juu ya uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 26, uliofanyika Juni 16, mwaka huu.
Licha ya taarifa hiyo kutofafanua wazi, ni wazi kuwa tukio la mlipuko wa bomu jijini Arusha la Juni 15 wakati wa kuhitimisha kampeni za udiwani eneo la Soweto, linatarajia kutawala kikao hicho wakati wa kujadili ajenda ya hali ya siasa nchini.
Hatua hiyo inatokana na mvutano uliojitokeza kati ya Jeshi la Polisi na viongozi wa CHADEMA ambao wanatamba kuwa na video inayomwonyesha mlipuaji wa bomu hilo ambaye anadaiwa kuwa askari polisi.
Hata hivyo, CHADEMA wamekataa kukabidhi ushahidi huo mikononi mwa polisi wakidai ni watuhumiwa, na hivyo wanamtaka Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru ya kimahakama itakayochunguza matukio yote ya mauaji ya kisiasa nchini.
Makene aliongeza kuwa kupitia agenda za kikao hicho, Kamati Kuu itajadili, kuazimia na kutoa msimamo wa chama juu ya masuala ya kitaifa na mengine yanayohusu maeneo mbalimbali.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya kufanikisha moja ya malengo ya chama ambayo ni pamoja na kutoa uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganaizesheni thabiti kwa ajili ya maendeleo endelevu ya jamii nzima ya Watanzania.

Bonyeza Read More Kuendelea



Mabaraza ya katiba kuanza
Wakati huo huo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba itaanza kuendesha mabaraza ya katiba ya wilaya Julai 12 huku ikitaka wajumbe wa mabaraza hayo kutoingiliwa na mtu, taasisi ama vyama vya siasa katika kutoa maoni yao.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema wanataka wajumbe hao wawe huru kutoa mawazo yao, ili yapatikane mawazo ya Watanzania ambayo yatachangia kuiboresha rasimu hiyo kabla ya kufikia kwenda kwenye Bunge la Katiba.
Alisema Tanzania bara kuna mabaraza 164 na Zanzibar mabaraza ya katiba ya wilaya 13 na kwamba tume itatumia siku 54 kuendesha mabaraza hayo nchi nzima.
Jaji Warioba alisema kuwa ili kufika sehemu zote, tume imejigawa katika makundi 14 na kila kundi litaendesha mikutano ya baraza ya wilaya katika mamlaka za serikali za mitaa 12 au 13.
Alisema kila mamlaka ya serikali za mitaa, mikutano yote ya mabaraza ya katiba ya wilaya itaanza saa 2:30 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.
Aidha, alisema kuanza kwa mabaraza hayo ya wilaya kutaenda sambamba na mabaraza ya wazi ambayo yataendeshwa na taasisi mbalimbali.
Alisema mabaraza hayo yameruhusiwa kuanzia Juni mosi mwaka huu na yametakiwa kuwasilisha maoni yao ifikapo Agosti 31.
Alieleza kuwa mabaraza hayo yatajisimamia na kujiendesha yenyewe kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na tume.
Alitoa wito kwa wananchi na wadau wengine kutumia fursa hiyo kutoa maoni na mapendekezo yao ambayo yatasaidia kuiboresha rasimu.
“Tume itapokea maoni na mapendekezo yote ambayo yatakuwa na lengo la kuiboresha rasimu ambayo italeta umoja wa kitaifa na sio kuwagawa Watanzania.
“Tumeona maoni mengi yametolewa tokea ilipozinduliwa rasimu ya awali, lakini tungezidi kuwaomba wasiishie kutoa maoni na hofu zao bali waisaidie tume kutoa mapendekezo ambayo yataisadia kuwapatia Watanzania katiba bora,” alisema.
Pamoja na hayo, alisema tume itaendesha mabaraza ya katiba mawili ya watu wenye ulemavu Mjini Magharibi, Zanzibar na mkoani Dodoma.
Uendeshaji mabaraza
Jaji Warioba alisema tume imetayarisha mfumo wa uendeshaji wa mikutano hiyo ambao utatoa ushiriki mpana kwa kila mjumbe kuchangia na kutoa mawazo yake kwa uhuru na uwazi.
Alisema mikutano hiyo si ya kupiga kura bali kujadili na kutoa hoja ambazo  zitakuwa na msingi  kwa maslahi ya taifa.
“Kila baraza litakutana kwa siku tatu. Siku ya kwanza wajumbe wataelezwa madhumuni ya mkutano, utaratibu wa uendeshaji wa mikutano na baadae wajumbe wataelezwa rasimu ya katiba kwa muhtasari kwa kila sura ya rasimu. Baada ya kuipitia rasimu wajumbe watagawanywa katika makundi manne.
“Siku ya kwanza na ya pili wajumbe watapitia, kuijadili na kuitolea maoni rasimu ya katiba kwenye makundi yao. Baada ya majadiliano siku ya tatu kila kundi litawasilisha maoni na mapendekezo yao mbele ya mkutano wa wajumbe wote, na wajumbe wengine ambao hawakuwa kwenye kundi watatapata fursa ya kuchangia maoni,” alisema.
Ratiba ya mikutano
Alisema kundi la kwanza litaanzia Mkoa wa Kagera (Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo), kundi la pili mkoani Shinyanga (Kishapu), kundi la tatu mkoani Mara (Tarime), kundi la nne mkoani Kigoma (Kakonko) na  kundi la tano litaanzia mkoani Tabora (Igunga).
“Kundi la sita litaanzia mkoani Lindi (Lindi mjini), kundi la saba mkoani Arusha (Ngorongoro), kundi la nane mkoani Kilimanjaro (Siha), kundi la tisa litaanzia mkoani Tanga (Korogwe),” alisema.
Aliongeza kuwa kundi la 10 litaanzia mkoani Kusini Unguja (Kusini Unguja), kundi la 11 mkoani Mbeya (Mbarali), kundi la 12 mkoani Rukwa (Nkasi), kundi la 13 mkoani Mtwara (Mtwara/Mikindani) na kundi la 14 litaanzia Njombe (Ludewa).
Kuhusu mapendekezo ya serikali tatu, Jaji Warioba alisema wamependeleza suala hilo kutokana na maoni ya wananchi, na pia suala hilo kujadiliwa kwa zaidi ya miaka 30 sasa.
Alisema kutokana na hali halisi ilivyo, wamependeleza serikali tatu ili kila upande (Zanzibar na Bara) uwe na mamlaka ya kufanya mambo yake.
Hata hivyo, alisema bado kuna nafasi ya kulibadili suala hilo iwapo wananchi watatoa hoja nzito.

No comments:

Post a Comment