MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa CCM, Sophia Simba amesema anahofia CHADEMA wanaweza kunyakua Jimbo la Babati Mjini au Vijijini.
Simba alisema CHADEMA inaweza kufanya hivyo iwapo viongozi na wanachama wa CCM watabweteka na kutowahamasisha watu wengi kujiunga na chama hicho tawala.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa CCM Mkoa wa Manyara kabla ya kuanza ziara yake ya siku tatu wilayani Babati.
Simba alisema viongozi na wanachama wa CHADEMA wanajituma katika kufanya kazi zao kichama, hivyo ni vema CCM wakaacha mazoea ya kuhamasisha kila chaguzi zinapokaribia.
“Mnawaona wenzetu wa CHADEMA wanavyohangaika huko kwa wananchi kutafuta wapiga kura kwa nguvu, na hii inaleta wasiwasi kwamba ikifika mwaka 2015 wanaweza hata kunyakua Jimbo hapa Babati, aidha Mjini au Vijijini,” alisisitiza Mwenyekiti huyo.
Alisema ili kuifanya CCM iwe imara ni lazima viongozi wa jumuiya zote ikiwemo ya vijana kuhamasisha watu kujiunga.
Simba alisema uhamasishaji huo ikibidi uendane na wanachama hao kutotoa ada za uanachama ili kuwavutia wengi zaidi.
“Tafuteni wanachama kwa nguvu zenu zote, ikibidi hata msiwalazimishe kulipa ada za chama na kuwaita wanachama wafu kwani mkiwaita wafu wataenda kwa wenzetu wa CHADEMA wanakochukuliwa bure,” alisema Simba.
Alisema miongoni mwa sababu zilizokifanya chama hicho kishindwe kwenye chaguzi ni kutowajibika ipasavyo katika uhamasishaji wa kutoa mwamko wa kisiasa kwa wanachama wake.
Simba alisema hali ni tofauti kwa wapinzani wao ambao kila kukicha wamekuwa wakihahangaika kwa wananchi huku wakifanya mikutano mbalimbali ya kuwarubuni kisiasa.
Alisisitiza kuwa viongozi wasiwachukulie kimzaha mzaha wapinzani wao kwani wanafanya mikakati na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Tuache kufanya kazi kwa mazoea, tunapofikiria sisi ni chama tawala na kubweteka tukisubiri wakati wa kampeni tutaumia, wenzetu mnawaona,” alisema.
No comments:
Post a Comment