Monday, July 22, 2013

BAVICHA mwenyeji mkutano wa IYDU

BARAZA la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), linatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa Bodi ya Umoja wa Vyama vya Demokrasia Duniani (IYDU), utakaofanyika kuanzia Julai 25 hadi 30, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratias Munishi, alisema mkutano huo utafunguliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa na utafungwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe.
Alisema IYDU inayoundwa na mataifa 81, katika historia Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Hii ni heshima ya pekee kwa BAVICHA, CHADEMA, Vijana wa Tanzania na taifa zima kwa ujumla,” alisema.
Alisema baraza hilo litatumia mkutano huo kuwapatia washiriki fursa ya kujua kama demokrasia na mfumo wa vyama vingi nchini, tasnia ya habari na nafasi yake katika maendeleo ya demokrasia, uzoefu wa kujenga jamii za kidemokrasia kupitia mabadiliko ya katiba.
Munishi alisema masuala mengine watakayojadili ni uwezeshaji na hali ya kiuchumi ya vijana wa Afrika kwa mtazamo wa sera za CHADEMA na fursa na changamoto kwa vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, alisema mkutano huo utakuwa ni fursa ya kuitangaza Tanzania katika sekta ya utalii kwa kuwa wanaamini kama taifa bado hawajafanikiwa kujitangaza vilivyo kupitia nyanja hiyo.
Alisema watoa mada katika mkutano huo watakuwa Mabere Marando (mwanasiasa mwandamizi na wakili wa kujitegemea), Jaji Thomas Mihayo (Jaji Mstaafu, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania), Wakili Francis Stolla (Rais wa Chama cha Mawakili Tanzania), John Mnyika (Makamu wa Rais mstaafu wa IYDU) na Jenerali Ulimwengu (Mwandishi mwandamizi).
Alisema ujumbe wa IYDU utapata fursa ya kuwa na mazungumzo na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Jumuiya ya Ulaya nchini na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC). Pia ujumbe huo utakutana na Spika wa Bunge la Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

No comments:

Post a Comment