Sunday, June 23, 2013

Tofauti ya bajeti ya serikali na CHADEMA

WIKI hii ilikuwa ya wabunge kuijadili bajeti kuu ya serikali iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, William Mgimwa.
Lakiti tofauti na utaratibu wa miaka yote, bajeti ya kambi rasmi ya upinzani bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haikuweza kusomwa bungeni kutokana na wabunge wote wa chama hicho kutokuwepo.
Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe aliyepaswa kusoma bajeti hiyo, naye aliongozana na wenzake mkoani Arusha kuomboleza vifo vya wafuasi wa chama chao waliolipuliwa na bomu wiki iliyopita.
Licha ya bajeti hiyo kutowasilishwa bungeni na kuingizwa kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard), CHADEMA waliona vyema waisambaze kwenye vyombo vya habari na mitandoo ya kijamii ili wananchi waone mawazo na mapendekezo yao mbadala.
Kwa kifupi CHADEMA imeainisha vyanzo vingi vipya vya mapato, vipaumbele na kufuta misamaha ya kodi zisizo na tija kwa taifa.
Zitto anasema kutokana na ongezeko kubwa la matumizi yasiyo ya lazima katika bajeti ya serikali, kambi rasmi ya upinzani imependekeza kupunguza asilimia 30 ya gharama za posho za vikao, semina, usafiri, viburudisho, mafuta na vilainishi.
Katika mchanganuo huo, Zitto alisema wanalenga kuondoa mikopo yenye masharti ya  kibiashara ili kulipunguzia taifa mzigo wa madeni wakati bajeti ya serikali ni yenye mikopo ya sh trilioni 1.156 yenye masharti ya kibiashara.
“CHADEMA inajikita katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo kwa kutenga zaidi ya asilimia 41 ya mapato ya ndani kugharimia miradi ya maendeleo, huku CCM inapingana na  mpango wa maendeleo wa taifa kwa kutenga asilimia 22.4  kinyume na matakwa ya mpango wa serikali ambao unahitaji asilimia 35.
“Bajeti yetu imeanzisha kodi maalumu ya michezo na Wakala wa Maendeleo ya Michezo wakati ile ya Serikali ya CCM haijali michezo na wala sio kipaumbele chake,” alisema.
Zitto anaongeza kuwa CHADEMA inalenga kulipa pensheni kwa wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea huku bajeti ya serikali haina mfumo wa pensheni kwa wazee.
Alisema kuwa wanapendekeza kushusha kiwango cha chini cha kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 14 hadi 9, lakini serikali katika bajeti yake imeshusha kodi hiyo kwa asilimia moja.
Zitto katika mchanganuo huo wa utofauti wa bajeti ya CHADEMA na ile ya serikali, anaongeza kuwa wanakusudia kuondoa matumizi yasiyo ya lazima kwa asilimia 30 wakati serikali ina matumizi yasiyokuwa ya lazima sh bilioni 214.
“Bajeti yetu inajitegemea kwa makusanyo ya mapato ya ndani  ya  asilimia 75.8, ile ya serikali ni tegemezi kwa asilimia 37.8 kutokana na kukopa kwa kiwango kikubwa.
“Sisi bajeti yetu ina punguzo la misamaha ya kodi na kufikia asilimia moja ya pato la taifa, serikali ina misamaha ya kodi  kiasi cha asilimia 4.3 ya pato la taifa, sawa na sh trilioni 1.922,” alisema.
Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alionesha kuwa CHADEMA itakabiliana nao kwa bidhaa muhimu, kwamba bajeti ya serikali ya CCM hazingatii mfumuko wa bei.
Alisema kuwa wakati CHADEMA wakionesha maslahi bora kwa wafanyakazi kwa kuongeza kima cha chini cha mshahara kuanzia sh 315,000, serikali ina kima cha chini cha sh 170,000 kisichoendana na gharama za maisha kwa sasa.
Zitto alifafanua kuwa bajeti yao inafuta ongezeko la kodi kwenye mafuta ya dizeli na petroli, huku ile ya serikali inaongeza kodi kwenye mafuta; dizeli asilimia 6.1 na petroli asilimia 8.5.
“Tutaondoa ongezeko la kodi kwenye ngano na hivyo bidhaa za ngano kama mikate, maandazi, chapati kutopanda bei, wao serikali wameongeza bei ya ngano kwa asilimia 10 na hivyo kutowajali wananchi wa kipato cha chini wanaotumia bidhaa hizi kwa wingi.
“Tunasema CHADEMA inafuta ongezeko la kodi kwenye matumizi ya simu za mkononi, lakini Serikali ya CCM inaongeza kodi kwenye simu za mkononi na hivyo mtumiaji kutakiwa kulipa kodi/tozo/ushuru wa asilimia 36.5,” alisema.
Zitto alivitaja vyanzo vyao vya mapato kuwa ni kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, marekebisho ya kodi za misitu na kupunguza misamaha ya kodi.
Pia watatoza kodi ya asilimia 0.5 kwenye mauzo na ya asilimia moja ya manunuzi ya nje kwa ajili ya kujenga reli na kuzuia ukwepaji kodi unaofanywa na kampuni za kimataifa.

Bonyeza Read More Kuendelea



Pinda  awataka polisi wapige tu
Wakati taifa likiwa kwenye moto wa vurugu za kisiasa, kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekoleza moto akivitaka vyombo vya dola kuendelea kuwapiga wananchi wanaokaidi amri wanazopewa, akisema kuwa hakuna namna nyingine, serikali imechoka.
Pinda alitoa kauli hiyo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyehoji kama serikali iko tayari kutoa tamko kuhusu vurugu zilizotokea jijini Arusha, Mtwara na maeneo mengine pamoja na hatua ya vyombo vya dola kutumia nguvu.
Alijibu swali hilo akisema kuwa suala la amani linawagusa wote, kwamba jukumu ni kwa viongozi wa kisiasa. Alifafanua kuwa kama viongozi wa kisiasa hawatafika mahali wakakubaliana bila kujali vyama vyao nchi itafika pabaya.
“Ninyi wote ni mashahidi CHADEMA waliposhindwa uchaguzi, walikuja hapa waziwazi wakasema kuwa watahakikisha nchi haitatawaliki. Sasa mheshimiwa Mangungu inawezekana ndio mwendelezo wa utekelezaji wa kauli hizo,” alisema.
Pinda alifafanua kuwa kwa upande wa serikali lazima wahakikishe kwamba wale wote wanaojaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile kazi waliyonayo ni kupambana kweli kweli kwa njia zozote zinazostahili.
“Mimi naomba sana Watanzania maana kila juhudi zinakoonekana zinaelekea huko tunapata watu wengine wanajitokeza kuwa mara unajua…unajua. Acheni serikali itimize wajibu wake kwa sababu jambo hili ni la msingi na wote tulilinde kwa nguvu zetu zote,” alisema.
Aliongeza kuwa kila Mtanzania ajue kwamba siku moja nchi hii ikiingia kwenye vurugu hakuna mshindi, na hasa watakaoumia zaidi ni watoto na akina mama, hivyo wote lazima wahakikishe wanasimamia amani.
“Mheshimiwa Mangungu umeanza vizuri, lakini hapa unasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, unaambiwa usifanye hiki ukaamua wewe kukaidi, utapigwa tu,” alisema.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa hakuna namna nyingine, maana lazima watu wakubaliane na serikali kwamba nchi hii wanaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ni jeuri zaidi, watakupiga tu na mimi nasema wapigwe tu maana hakuna namna nyingine, tumechoka,” alisema.
Alitolea mfano wa mbunge mmoja kutoka Mtwara, akisema naye alikuja bungeni kulalamika kuwa vyombo vya dola vinatesa watu.
“Lakini mimi nilisema hapa kuwa tunataka kurejesha amani Mtwara, na nikawaambia Watanzania kuwa tunaombeni radhi katika hili kuwa tukianza kazi wako watu watajitokeza na kusema vyombo vya dola.
“Mtwara pale tuna orodha ya watu ambao wanasemekana ndio vyanzo vya matatizo na vurumai, sasa unataka tusiwakamate? Lazima tuwakamate na kama katika kuwakamata wakifanya jeuri watapigwa tu kabla ya kuwapeleka tunakotaka kuwapeleka,” alisema.
CUF wakwama kuipindua CHADEMA
Wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) wamekwama kufanya mapinduzi ya kuongoza kambi rasmi ya upinzani bungeni, wakidai kuwa chama cha CHADEMA kinachoongoza kambi hiyo hakimo bungeni kwa wiki nzima.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwan (CUF) ambaye aliomba mwongozo wa spika, akisema kwa saa 96 sasa kambi ya upinzani iko wazi, hivyo CUF wanatangaza rasmi kwamba kuna mapinduzi ndani ya Bunge kwa kambi hiyo kuongozwa na wao.
Kauli ya Barwan ambaye alikuwa amekalia kiti cha kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA) iliibua vicheko kwa wabunge wote ukumbini.
Hata hivyo, katika mwongozo wake, Spika Anne Makinda alifafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni, kambi rasmi ya upinzani ni wabunge wote wa upinzani, na kuongeza kuwa hata hivyo vyama hivyo vimekuwa na misimamo tofauti katika kuongoza kambi hiyo kulingana na uwiano wao.
Alisema kwa sasa kambi hiyo inaongozwa na CHADEMA na kwamba licha ya CUF kukidhi kigezo cha kuwa na asilimia 12.5 ya wabunge na hivyo kuwa na sifa za kuunda kambi ya upinzani, lakini wanaoiongoza (CHADEMA) hawajatangaza kuiacha kazi hiyo.
Barwan alikaa sehemu ya Mbowe huku Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) naye alikalia kiti cha Mnadhimu Mkuu wa Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kuonesha kuwa wabunge wa chama hicho wametwaa kambi kutoka kwa CHADEMA ambayo wabunge wake wote hawakupo bungeni kwa wiki nzima.
Wabunge wa CHADEMA wakiongozwa na Mbowe walikuwa jijini Arusha kuzika na kuwafariji wafuasi wa chama chao waliofariki na kujeruhiwa katika tukio la mlipuko wa bomu lililotokea wiki iliyopita.
Kafulila adai CC ya CCM imechoka
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) ametoa mpya kwa kuiponda Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema kuwa kwa miaka 50 ya uhuru imeshindwa hata kumaliza kero ya wanafunzi kuketi chini.
Alisema kuwa chama tawala serikali yake ushauriwa na Kamati Kuu, kwamba kwa CCM kwa kipindi chote imechoka na hivyo kushindwa kuweka mikakati ya kuikwamua nchi.
Kafulila alitoa hauli hiyo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 akisema kuwa bajeti haifafanui ni ajira ngapi zitazalishwa na umasikini utapunguzwa kwa kiwango gani.
“Ukiangalia bajeti ya wenzetu Kenya wanaonesha kuwa wanataka kupeleka kompyuta mpakato (laptop) kwa kila mwanafunzi wa shule ya msingi, sisi kwa miaka 50 ya uhuru tumeshindwa kununua hata madawati ya kutosha, bado wanafunzi wetu wanakaa chini,” alisema.
Kafulila alifafanua kuwa Kenya wamesema kuwa kwa mwaka ujao wanataka kupunguza umasikini kwa asilimia 10 na kutengeneza ajira milioni moja, lakini bajeti yetu haioneshi mambo hayo yatafanyikaje.
“Chama tawala kamati kuu yake ndiyo inaishauri serikali na kwa CCM kamati kuu inakutana mara nne kwa mwaka, ina maana kwa miaka 50 imekaa mara 200, lakini hata madawati mmeshindwa, kwanini tusiwaeleze kuwa mmechoka?” alihoji.
Kuhusu kodi, Kafulila alisema kuwa serikali inapoteza mapato mengi kutokana na misamaha ya kodi kwa makampuni makubwa na badala yake imekuwa ikiwakandamiza masikini kwa kuwaongezea kodi kwenye bidhaa.
“Serikali hii haikusanyi kodi kwa matajiri, ndiyo maana hata hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa serikali ya kifisadi haikusanyi kodi, bali inabaki kukimbizana na masikini kwa kuwatoza ushuru wakati wenye migodi na mahoteli wakiachwa,” alisema.
Alisema kuwa sheria ya kuyabana makampuni hayo kulipa kodi ilishafanyiwa marekebisho ila kinachochelewesha ni kutungwa kwa kanuni, na hivyo kutishia kuwa endapo serikali haitaleta kanuni hizo watawashawishi wananchi wao waache kulipa ushuru.
CCM wajishuku mlipuko Arusha
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinazidi kuhaha kikijaribu kujinasua katika tuhuma za kuhusika na shambulio la mlipuko wa bomu jijini Arusha, ambapo sasa makada wake wawili juzi walilazimika kutumia Bunge kukitupia lawama chama CHADEMA.
Makada hao ni Naibu Katibu Mkuu (Bara), Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia ambao walidai kuwa CHADEMA ndio wamekuwa wakihusika na vurugu zote zinazohusisha mauaji nchini.
Kauli za viongozi hao zinakuja ikiwa ni takribani siku tano tangu Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye kudai kuwa wanao ushahidi wa kutosha kuwa CHADEMA iliandaa na kuratibu shambulio hilo liloua watu watatu na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.
Katika madai yake, Mwigulu alianza kusema kuwa jambo la usalama wa nchi hii amekuwa akiliongelea kwa haraka haraka na hivyo watu wamekuwa hawamwelewi.
“Leo naomba niliseme kwa utaratibu, jambo la usalama nimekuwa nikilisema na kuomba kama Elia aliyemwambia mtumishi wake kuwa anamwombea Mungu amfungue macho ya ki-Mungu ili aone jinsi yeye anavyoona.
“Jambo limetokea kama hili la Arusha, nimeyaongea sana mambo haya na sasa hivi ilipotokea mimi nitasema tena na wenzetu nikiwasema mara wanasema wataenda jimboni. Nawashauri wasiende tu jimboni bali wajenge kabisa makao makuu ya chama chao,” alisema.
Mwigulu ambaye alikuwa akishangiliwa na baadhi ya wabunge na baadhi ya mawaziri wakiwemo William Lukuvi, George Mkuchika, Ghasia, Mery Nagu na wengine alisema anausema ukweli.
“Ni lazima tuwaze tuvuke mipaka, kuna mambo ambayo yanawezekana kabisa yakawa yamejificha pale. Watu wanaangalia, wanaojitoa ufahamu wanafikiria CCM inaweza kushiriki.
“Mimi niwaambie CCM hata bila kushiriki ni moja kwa moja inawekwa kwenye lawama jambo kama hilo likitokea. Ila CCM haina ushiriki katika jambo kama hili kwa sababu ndio watu wake kupitia serikali yake inatakiwa kuwahakikishia usalama,” alisema.
Alisema kuwa ni lazima waangalie maana wengine waliojaa ushabiki linapotokea jambo wanakwenda moja kwa moja kuwa inawezekana CCM imeshiriki.
“Sisi tunakimbilia tu CCM ndio imejaa midomoni mwa watu, lakini hoja nyingine Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, hivi wale ambao hawatutakii mema hamjajua eneo wanaloweza wakagusa?” alihoji.
Huku akinukuu ripoti ya Jukwaa la Wahariri nchini kuhusu utekwaji wa Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda, Katibu huyo alidai CHADEMA imetajwa kuwa ndio inahusika na matukio hayo ya utekeaji kwa kushirikiana na maofisa usalama wasio waadilifu.
“Niliwahi kulisema hili kuwa kuna mambo mengine yanafanyika kwa hujuma na tumeziona hizo hujuma, lakini watu wengine wanawahi kuamini haraka.
“Lakini hawa wenzetu kama waliwahi kumvalisha raia jezi ya jeshi na alihukumiwa, wanashindwaje kila wakati wanasema polisi… polisi. Tunashindwaje kuamini kama wanaweza kumvalisha mtu nguo za polisi na akafanya yale?” alihoji.
Mwigulu bila kujali kuwa analidanganya Bunge, aliamua kupotosha hata taarifa ya Polisi Mkoa wa Morogoro kuhusu tukio la kifo cha kijana Ali Zona kilichotokea wakati wa maandamano ya CHADEMA, akidai taarifa zilizopo chama hicho ndicho kilihusika.
Hawa Ghasia ambaye vile vile ni mjumbe wa NEC naye akadai kuwa  CHADEMA ndicho kinahusika na matukio ya vurugu nchini. Kwamba kimechochea vurugu Mtwara, Mwanza, Mbeya, Morogoro na sasa Arusha ili maeneo hayo yasipate maendeleo.

Na Edson Kamukara

No comments:

Post a Comment