Sunday, June 23, 2013

CCM inahusika

MAZINGIRA ya kabla na baada ya tukio la mlipuko wa bomu lililotokea mkoani Arusha katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), uliofanyika wiki iliyopita katika Uwanja wa Soweto na kusababisha vifo vya watu wanne, yanaonyesha uwezekano mkubwa wa baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuhusika, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Duru za kisiasa kutoka ndani na nje ya chama hicho, zimebaini kuwa CCM inahusika na mlipuko huo ikiwa ni mwendelezo wa harakati za chama hicho tawala kutaka kuiaminisha jamii kwamba CHADEMA ni chama cha  vurugu, ugaidi ili kukipunguza kasi kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Matukio kadhaa, yakiwemo mashitaka ya ugaidi yaliyofunguliwa dhidi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare ambayo baadaye yalifutwa na mahakama, huku Naibu Katibu Mkuu CCM, Mwigulu Nchemba akitamba kuhusika na mkakati huo, yanadaiwa kuwa sehemu ya mpango wa kukisambaratisha chama hicho cha upinzani.
CCM kwa kutumia askari polisi wasio waaminifu wanatajwa pia kuhusika katika mauaji ya muuza magazeti mkoani Morogoro wakati wa maandamano ya CHADEMA kwa lengo lilelile la kutaka kuiaminisha jamii kwamba chama hicho ni cha kigaidi.
Mauaji ya kinyama ya mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel ten, Daud Mwangosi wakati polisi wakipambana na wafuasi wa CHADEMA mkoani Iringa, yalikuwa na lengo la kukihusisha chama hicho, lakini ushahidi wa picha ulioonyesha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakimsulubu mwandishi huyo, ulimaliza ubishi huo.
Katika tukio la Arusha, moja ya ushahidi mpana wa kuihusisha CCM na tukio hilo ni mkanda wa video ilionao CHADEMA ambao chama hicho kinadai kuwa unamuonyesha mtu anayedaiwa kuhusika kurusha bomu hilo, akikimbilia ndani ya gari la polisi na kisha kuendeshwa kwa kasi kutoka eneo la tukio, huku polisi wakifyatua risasi kupambana na wananchi waliokuwa wakimfukuza mtuhumiwa huyo.
Mashuhuda wamedai kumwona na kumtambua mtu aliyehusika na tukio hilo, lakini wanasema walishindwa kumkamata kwa madai ya kushambuliwa kwa risasi na polisi.
Mlipuko huo ulitokea katika Uwanja wa Soweto kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani jijini humo na kusababisha vifo vya watu wanne na majeruhi zaidi ya 100.
Mlipuaji huyo anadaiwa kuvalia shati la kijivu lenye mistari myeusi na suruali ya jinzi yenye ya rangi bluu, na ni mtu wa makamo ambaye anadaiwa kutumika na CCM.
Mmoja wa majeruhi wa tukio hilo ambaye pia ni mlinzi wa CHADEMA, alisema shahidi wa kwanza kumwona mtuhumiwa huyo ni mama mmoja aliyekuwa karibu nae.
Alisema baada ya mlipuko huo, mama huyo alimfuata mlinzi na kumwonyesha kwa kidole mtuhumiwa wa mlipuko huo ambaye anadaiwa kuwa mmoja wa askari.
Mlinzi huyo ambaye alipigwa risasi za mguuni na kifuani wakati akimkimbiza mtu huyo, alisema bomu hilo lililipuka mara baada ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia na kushuka jukwaani.
Maelezo ya mlinzi huyo yanafanana na yaliyotolewa na majeruhi mwingine ambaye alisema kuwa alimwona mtu aliyelipua bomu “akiingia kwenye gari la polisi”.

Bonyeza Read More Kuendelea



Kauli ya Mtikila yaibua utata
Sababu nyingine inayotajwa kuihusisha CCM na tukio hilo ni jinsi inavyotoa kauli za kujihami kuanzia kwa mawaziri wake bungeni na hata kutumia vyama vingine vya siasa kuikandamiza CHADEMA.
Moja ya chama kinachodaiwa kutumiwa na CCM katika tukio hilo ni Democratic Party (DP), ambacho kilitoa tamko lililoishutumu CHADEMA kuhusika na mlipuko wa mabomu Arusha.
Tamko hilo la DP inayoongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila, lilisambazwa kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kupitia barua pepe ya CCM ambayo ni CCMtanzaniacontentsfolder@gmail.com, kabla ya mwenyewe kulisoma kwenye mkutano wake na waandishi wa habari.
Haijulikani sababu hasa za CCM kujitolea kulisambaza tamko hilo kwa haraka, tena kwa wahariri wote wa habari wakati halikuwa lao huku Mtikila alikuwa na uwezo wa kulisambaza yeye mwenyewe kupitia waandishi wa habari aliowaita.
Akizungumzia suala hilo, Mtikila alisema hata yeye anashangaa kwanini tamko lake limesambazwa kupitia barua pepe ya CCM.
“Mimi pia nashangaa, maana baada ya kuandaa tamko langu, nilimpa mtu akatoe nakala ili niwape waandishi wa habari, lakini kabla huyo mtu hajatoa nakala na kurudi kwangu, nilipigiwa simu kuambiwa tamko langu lilikuwa limesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, na kutumwa kwa wahariri wengine kupitia baruapepe ya CCMtanzaniacontentsfolder@gmail.com,” alisema Mtikila.
Mtikila pia amepata kutumika na CCM kwenye uchaguzi mdogo Tarime ambapo katika mikutano yake ya kampeni alikuwa akiwaambia wana Tarime kwamba mbunge wao wa zamani, marehemu Chacha Wangwe, aliuawa na CHADEMA.
Katika tamko lake la juzi, Mtikila alisema mlipuaji wa bomu la Arusha hakukusudia kumuua Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, maana kama angalikuwa anahitaji kufanya vile angerusha bomu akiwa jukwaani.
Alisema bomu hilo lililengwa kwa walalahoi ili CHADEMA wapate kura za huruma kwa kuwa chama hicho hakikubaliki Arusha na kulikuwa na dalili za kushindwa katika uchaguzi huo.
Kauli ya Mwigulu kabla ya bomu
Siku moja kabla ya mlipuko huo wa bomu – Juni 14, Mwigulu alifanya mkutano wa kampeni  katika eneo la Kimandolu na kuwaonya watu wa Arusha  kwamba wasipoichagua CCM, watakufa.
“CCM baada ya kufanya tathimini walijua kabisa watashindwa, mbinu iliyobaki ilikuwa kuvuruga uchaguzi ili utakaporudiwa wananchi wasiichague CHADEMA kwa vile itakuwa imehusishwa na ugaidi,” alisema Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

No comments:

Post a Comment