Sunday, June 16, 2013

Nani anayefanya Uharamia huu?

HAKUNA kificho tena, sasa nchi yetu ya Tanzania inatafsirika ni ya Kigaidi!
Lakini nani anayefanya Uharamia huu? Nani anauruhusu ufanyike? Hata kama Serikali imeshindwa, Hivi Mungu naye anaweza kushindwa kumshughulikia huyu anayemwaga damu za watu zisizo na hatia? Hashindwi!.
Najiuliza kila yanapotokea matukio kama mawili ya Arusha, ambapo Mabomu yalitupwa na mtu makusudi, kiasi cha kuua na kujeruhi watu  waliofanywa kuwa Vilema bila kutarajia!
Anayefanya hayo ana Wazazi, ndugu na Jamaa zake? Je mtu huyu ana Mke  au Mume na Watoto? Huyu mtu kweli ana Wakwe zake? Ana uhai na anapumua kama wandamu? Maana huyu si wa kawaida! Labda ni Shetani anayekunywa damu za watu!
Namshangaa mtu huyu asiyeona huruma damu zikimwagika, viungo vya watu vikisambaratika ardhini na damu zao zikidonolewa na ndege, Kuku na wadudu, huku yeye akifurahi moyoni mwake!
Labda mtu huyu hana makazi mbinguni (Ahera), ameshakataliwa na Mungu, hivyo anazungukazunguka kama simba aungurumaye ili kutafuta Mtu ammeze! Na kwa hasira ya kukataliwa, ndiyo maana anaamua kufanya uharamia akidhani atawapata wa kwenda nae. Amekosa!
Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema, “Mtu akisha kuonja kula Nyama ya Mtu, akaona ni tamu, hataacha, ataendelea kula tu hata akivimbiwa hatatosheka” inaonekana Uharamia wa kutafuna Nyama za watu, hajatosheka!
Vyombo vya Dola, Wenyeviti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya, Mikoa na Taifa, inaonesha wameshindwa kudhibiti uharamia huu unajitokeza kila siku inapoitwa leo. Ushahidi wa kushindwa, ni vitendo hivyo kujitokeza pamoja na kuwepo walinzi.
Tujiulize! Je bado Vyama na Wananchi, wawe na Imani navyo na kuomba ulinzi kwao? Kama watu wanafanya uharifu wa uharamia wa kigaidi mbele ya vyombo hivyo? Kama uharamia umefanywa machoni mwao, alaumiwe nani?
Tusemeje! Kama Uharifu na Uharamia wa namna hii unaendelea kufanywa Machoni mwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Vyombo vyake vya Usalama na kumnusuru Mharifu, wananchi tuwe na Imani Ipi?
Awali Bomu lililolipuka katika mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa, tulisema ni bahati mbaya. Je hili ambalo ulinzi umeombwa!
Nia Nzuri ya Serikali ya CCM kutaka mikutano ya hadhara inapofanyika taarifa zitolewe kwa vyombo vya Usalama, ni kusudi likitokea Jambo, vyombo vya usalama viwe na sababu ya kuulizwa na kuwajibika kukabiliana nalo!
Sasa vibali viliombwa na ruhusa ikatolewa, uharamia umetokea mikononi mwa ulinzi wa vyombo hivyo! Je ashikiwe bango nani? Basi kikosi kizima kilichohusika na ulinzi kwenye mkutano huo viwajibike pamoja na mkuu wao! Maana vimeshindwa kulinda.
Aidha kabla hatujailaumu Serikali na CCM, CCM iiwajibishe Serikali na Serikali iliwajibisha Polisi na Vyombo vyake, maana vimeshindwa kutekeleza wajibu wake na kusababisha maisha ya watu kupotea bila ya wao kumpoteza Mharamia! Lau mmoja wao!
Ni rai yangu kwa wananchi, Ninyi ndio Walinzi wazuri wa Amani ya Tanzania, hivyo nawashauri wasidanganyike na Kamga na Kofia na lolote, iwapo wataamua Kuta za Yeriko zianguke, basi wanaweza 2015 wakazunguka Yeriko mara Saba na Kulia Huleee! Kuta zitaanguka!
Nasema nikirejea! Mungu hashindwi kumpata anayesababisha vilio vya watanzania vitoe machoni mwao!

No comments:

Post a Comment