Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni leo itawasilisha bajeti yake kivuli ya serikali ya 2013/2014 huku suala la kukua kwa deni la Taifa na Serikali kukosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato yakiwa ni mambo yanayotarajia kuibuliwa katika hotuba hiyo.
Bajeti hiyo ilisomwa Alhamis wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, huku Serikali ikiomba kuidhinishiwa Sh. trilioni 18.2 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi kawaida.
Kwa mujibu wa Dk. Mgimwa, vipaumbele katika bajeti hiyo ni maji, nishati, uchukuzi, kilimo, elimu na kuongeza pato.
Mbali na ubunifu wa vyanzo vya mapato, kambi hiyo inatarajiwa kuzungumzia suala la ongezeko la ushuru katika bei ya mafuta, misamaha ya kodi, ufisadi na matumizi makubwa ya Serikali, masuala ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na Watanzania wengi.
Deni la Taifa hadi kufikia Machi mwaka huu, lilikuwa limefikia Sh. bilioni 23,673.53 ikilinganishwa na deni la taifa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo kilikuwa ni Sh. bilioni 20,276.6.
Kutokana na kukua kwa deni hilo, kambi hiyo inatarajia kueleza mbadala ya kupunguza deni hilo ikiwamo kuitaka serikali kuacha kukopa hovyo bila kuwapo sababu za msingi.
Kwa upande mwingine, Kambi ya Upinzani inaona licha ya kuwepo kwa fedha za kutosha, suala la kuthibiti matumizi ya serikali katika masuala yasiyo ya lazima nalo ni muhimu.
Kambi hiyo pia imekuwa ikilalamikia kuhusiana na ufisadi wa fedha za umma, eneo ambalo limekuwa likisababisha hasara kubwa kwa serikali.
Kambi hiyo vile vile itaibua wigo wa vya mapato serikali badala ya kuendeleza utamaduni wa kutegemea soda, bia, sigara, mafuta na magari.
Tayari Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alikaririwa na gazeti hili akisema bajeti hiyo haina jipya na kwamba itamuongeza makali ya maisha mwananchi wa kawaida kutokana na ongezeko la ushuru na tozo katika mafuta.
Alisema hiyo inasababishwa na Serikali kutokuwa na ubunifu katika masuala ya kodi na kubakia na vyanzo vile vile kama sigara, mafuta, vinywaji na magari.
Pia alisema suala la kupanda kwa ushuru wa magari litafanya walalahoi kushindwa kununua magari.
Bajeti hiyo ambayo kinachoonekana chanzo kipya cha mapato kuwa ni ushuru katika huduma za simu, itajadiliwa kwa wiki moja hadi Jumanne Ijayo wakati Waziri mwenye dhamana atakapohitimisha kwa kutoa majibu ya hoja mbalimbali zitakazotolewa na wabunge.
No comments:
Post a Comment