Tuesday, June 11, 2013

Mbunge ataka rais ashitakiwe asipotimiza ahadi

MBUNGE wa Viti Maalumu, Suzan Lyimo (CHADEMA), amesema marais wanaoshindwa kutekeleza ahadi zao mpaka wanapomaliza vipindi vyao vya uongozi washitakiwe.
Lyimo alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiuliza swali la nyongeza ambapo alisema wabunge wengi hususan wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanalalamika kwa kutotekelezwa kwa ahadi za marais na kutaka wapelekwe mahakamani walishindwa kufanya hivyo.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema katika ahadi za rais hakuna mtu wa kushitakiwa na kwamba ahadi zinazotolewa na hutekelezwa na serikali.
“Ahadi inayotolewa na rais utekelezaji ni jukumu la serikali na fedha inatoka serikalini haitoki mfukoni mwa rais sasa hapa hakuna wa kushitakiwa, kwani rais aliyepo madarakani akiondoka atakuja mwingine ambaye ataendelea na utekelezaji wa ahadi zilizobakia,” alisema Lukuvi.
Alisema serikali kwa kadiri ya uwezo wake imejitahidi kutekeleza ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa juu serikalini.
Awali katika swali la msingi Mbunge wa Mkinga, Dustan Kitandula (CCM) alitaka kujua hatua zilizochukuliwa hadi sasa katika utekelezaji wa ahadi ya rais ya kujenga Hospitali ya Wilaya ya Mkinga pia alitaka kujua ni lini utekelezaji wa ahadi za rais utakamilika.
“Wakati wa ziara yake wilayani Mkinga, rais aliahidi kujengwa haraka Hospitali ya Wilaya ya Mkinga kutokana na kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Maramba ili kitoe huduma za hospitali ikiwamo upasuaji, utekelezaji wa ahadi hizo umefikia wapi?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Seif Rashid, alikiri kwamba katika mwaka 2010 rais alipotembelea wakazi wa Mkinga aliahidi kupandisha hadhi Kituo cha Afya cha Maramba ili kiweze kutoa huduma za dharura lakini pia aliahidi kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkinga.
“Hata hivyo katika kutekeleza ahadi hizo serikali imetumia jumla ya sh milioni 132.1 kuboresha miundombinu ya Kituo cha Afya Maramba ili kiweze kupandishwa hadhi na kutoa huduma bora zinazoendana na hospitali,” alisisitiza naibu waziri huyo.
“Kazi zilizofanyika ni upanuzi wa eneo la kituo hicho kwa kuhamisha makazi ya watu wanne na kuwalipa fidia, kufanya ukarabati wa chumba cha upasuaji, kuweka upya mfumo wa umeme na maji taka, kununua kontena kwa ajili ya kutengeneza chumba cha mapokezi na kununua mashine ya dawa ya usingizi na mashine ya kufua nguo,” alisema Dk. Rashid.
Kuhusu ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mkinga, alisema imeshatoa sh milioni 221.4, ambapo sh milioni 21 zimetumika.
Aidha, alisema kwa sasa Kituo cha Afya cha Maramba kinatoa huduma zote muhimu isipokuwa upasuaji kwa wajawazito na chumba cha upasuaji kipo katika hatua ya mwisho ya ujenzi na kinatarajiwa kukamilika kabla ya Julai mwaka huu.

No comments:

Post a Comment