Sunday, June 16, 2013

Mbowe anusurika kuuawa kwa bomu

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amenusurika kuuawa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu, lililolipuka katika mkutano wa hadhara wa kampeni za udiwani mkoani Arusha.
Mbali ya Mbowe, viongozi wengine mbalimbali waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, walinusurika katika mlipuko huo wa bomu hilo lililorushwa katika Uwanja wa Soweto muda mfupi baada ya mwenyekiti huyo kumaliza kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni, Emanuel Kessy, jijini hapa.
Habari kutoka eneo la tukio zilisema kuwa watu kadhaa wanasadikiwa kufariki dunia na wengine zaidi 15 wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao ikiwamo miguuni na kichwani  wakiwamo watoto wawili wanaodaiwa kuvunjika miguu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabath, alithibitisha kuwa watu wawili waliuawa katika mlipuko huo na kulielezea tukio hilo kuwa ni kubwa na baya kuendelea kutoka mjini hapa.
Mwezi mmoja uliopita, mlipuko wa bomu kama hilo ulitokea katika Kanisa Katoliki Olasiti la Joseph Mfanyakazi na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Mmoja wa mashuhuda aliyezungumza na Tanzania Daima Jumapili muda mfupi baada ya mlipuko wa jana, alisema alijitokeza mtu ambaye hakujulikana anapotokea na kurusha bomu la mkono katikati ya umati na bomu hilo kutoa kishindo kikubwa.
Alisema baada ya mtu huyo kurusha bomu hilo baadhi ya wananchi na wafuasi wa CHADEMA walimuona, walianza kumkimbiza na kabla hawajamfikia polisi waliokuwa wameweka ulinzi katika eneo hilo waliingilia kati na kuzuia mtu huyo asifikiwe.
Bomu lililorushwa linadaiwa kuwa lilielekezwa katika jukwaa walilokuwa Freeman Mbowe na viongozi wengine ambao muda mfupi kabla ya tukio hilo walikuwa wameshuka jukwaani kwa ajili ya kuondoka katika eneo hilo.
Hali katika eneo la tukio ilikuwa mbaya baada ya damu kutapakaa sehemu mbalimbali ya uwanja wa Soweto na majeruhi zaidi ya 20 wakikimbizwa katika hospitali za jijini humo.
Wafuasi wa CHADEMA waliendelea kukakaa katika uwanja huo huku wakihanikiza kwa wimbo wa kukishutumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa kinawaua.
Chanzo kingine kilieleza kuwa katika majeruhi waliopelekwa katika Hospitali ya Mount Meru, mtoto mdogo ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema bomu hilo ni mbinu ya watu wanaohofia kushindwa katika uchaguzi huo na kuwataka wafuasi wao kutoka maeneo yasiyo na uchaguzi kujitokeza kwa wingi kulinda kura zitakazopigwa leo.
Hali katika Hospitali ya Mount Meru
Tanzania Daima Jumapili lilishuhudia majeruhi hao wakiingizwa na kutolewa katika Hospitali ya Mount Meru mara baada ya kutokea kwa tukio hilo lililotokea saa 11:40 muda mfupi baada ya Mbowe kumaliza kuhutubia wananchi wa kata hiyo na kumuombea kura mgombea huyo.
Katika Hospitali ya Mount Meru, umati mkubwa wa wafuasi wa CHADEMA ulifurika muda mfupi baada ya kutokea kwa tukio hilo, ambao wengi wao walionekana kushinikiza wauguzi wachache waliokuwepo hospitalini hapo kuwapatia majeruhi huduma ya kwanza.
Zoezi zima la kushinikiza wauguzi hao kuwapatia huduma majeruhi hao liligeuka baada ya baadhi ya wauguzi kujificha wakiogopa umati huo wa wafuasi wa CHADEMA, hivyo majeruhi kukosa huduma ya kwanza.
Hali hiyo iliwalazimu wafuasi wa CHADEMA kubeba majeruhi hao waliokuwa wakivuja damu katika miili yao kwa kutumia magari binafsi na kuwahamishia hospitali mbalimbali ikiwamo Hospitali ya Rufaa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri ya Seliani ya jijini hapa.
Mmoja wa wafuasi wa CHADEMA aliyejitambulisha kwa jina la Martin Lucas, alidai wakiwa katika Uwanja wa Soweto huku mkutano ukiendelea kwa amani na utulivu na Mwenyekiti wa CHADEMA alipomaliza kuhutubia na kushuka jukwaani akielekea kupanda gari lake tayari kuondoka, ghafla mlipuko mkubwa ulitokea katika jukwaa alilokuwa akihutubia.
“Ndugu mwandishi hii ni hujuma kabisa, mkutano ulifanyika kwa amani na utulivu wa kutosha, ghafla tukashangaa watu wanaanguka chini huku moshi mkubwa ukipaa juu,  sisi tulikuwa pembeni ya mti tukafikiri mwenyekiti wetu amepigwa bomu lakini haikuwa hivyo, yeye alishapanda gari na kuanza safari, watu wengi wameumia sana ndugu yangu,” alisema mfuasi huyo, Robert Kinabo.
Hadi tunakwenda mitamboni eneo lilipotokea mlipuko huo lilikuwa limezingirwa kwa alama ya tahadhari ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuwasubiri wataalamu wa milipuko kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa ajili ya kubaini aina ya mlipuko.

No comments:

Post a Comment