Sunday, June 16, 2013

Kivumbi CCM, CHADEMA leo

MBUNGE wa Hanang’, Manyara, Dk. Mary Nagu, amejikuta kwenye ulinzi mkali kutoka kwa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akidaiwa kutaka kutoa rushwa kwa wapiga kura wa Kata ya Bashnet, wilayani Babati.
Dk. Nagu ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwezeshaji na Uwekezaji), amekumbwa na balaa hilo usiku wa manane wa kuamkia jana katika Kijiji cha Guse alipokwenda kufanya kampeni za uchaguzi mdogo wa diwani, unaotarajiwa kufanyika leo.
Mbunge huyo akiwa na Mbunge wa Babati Vijijini, Jitu Soni, walizingirwa na wafuasi wa CHADEMA kwenye nyumba ya mkazi mmoja mjini hapa, wakimzuia asitoke kwenda kuonana na wapiga kura usiku huo kwa hofu kwamba alitaka kwenda kutoa rushwa.
Diwani wa Gisambalang’, wilayani Hanang’,  Masala Bajuta, aliliambia gazeti hili kuwa Waziri Nagu na mbunge huyo walilazimika kukaa kwenye nyumba hiyo, mali ya Petro Baha, hadi saa mbili asubuhi kwa hofu ya kushambuliwa na wafuasi hao wa CHADEMA.
“Bahati nzuri mipango yao ilishtukiwa na wananchi wapenda maendeleo na kuwatonya makamanda wa CHADEMA ndipo mpango wa kuwadhibiti ukaandaliwa na ilipofika usiku huo walizingirwa kwa lengo la kutoruhusiwa kutoka na kwenda kwa wananchi,” alisema Masala.
Diwani huyo alisema kuwa madiwani wengine waliokuwa katika sakata hilo ni pamoja na Diwani wa Gidahababie, Hilda Girei, Diwani wa Viti Maalumu Katesh Mjini, Juliana Songai na Diwani wa Viti Maalumu wa Masqaroda, Bailet Peter, kata zote zikiwa wilayani Hanang’.
Diwani huyo ambaye ni mratibu wa kampeni hizo alisema wakati tukio hilo likiendelea taarifa ziliwafikia polisi na kuwahi eneo la tukio ambapo wafuasi wa CHADEMA walipoulizwa, walisisitiza kuwa wana hofu kwamba Nagu na mbunge huyo wa CCM walikuwa na mpango wa kutoa rushwa.
“Hata wananchi wenyewe wa huku Bashnet hawajazoea kampeni za usiku na ndiyo maana siri yao ya kutaka kutoa rushwa usiku ikavuja, wawaache wananchi waamue siku ya kupiga kura wamchague kiongozi wanayemkubali kiutendaji na si kwa rushwa,” alisisitiza diwani huyo.
Masala alibainisha kuwa wafuasi hao wakiwa wameungana na wananchi waliwaruhusu polisi kuendelea na shughuli zao na kuwaahidi kumlinda Nagu na mbunge huyo hadi asubuhi.
Uchaguzi huo unaofanyika leo, unawashirikisha wagombea watatu ambao ni Nicodemas Gwandu (CCM), Alois Gwandu (NCCR - Mageuzi) na Laurent Tara (CHADEMA).
Wakati huo huo, vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Iringa wanadaiwa kuvamia kambi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuwapiga wafuasi wa chama hicho pamoja na kumjeruhi Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CHADEMA, Lunyiliko Nyaulingo.
Tukio la kuvamiwa kwa mzee huyo lilitokea jana katika Kata ya Nga’ng’ane, wilayani Kilolo wakati wafuasi wa CHADEMA wakijiandaa kwenda kwenye mkutano wa mwisho wa kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa udiwani unaofanyika leo.
Wavamizi hao wakiongozwa na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Elisante Kimaro, walisikika wakisema hawaogopi kufanya vurugu kwa kuwa polisi na mkuu wa Wilaya ya Kilolo wanajua kinachofanyika.
Mbali na kuvamia katika ya chama hicho, wafuasi hao wa CCM waliendeleza vurugu hadi katika mkutano wa CHADEMA uliokuwa ukifanyika katika Uwanja wa Mtakuja.
“Tunamaliza leo, wakubwa wetu wanafahamu kuwa tumekuja kufanya nini huku, leo ama zenu ama zetu,” zilisikika sauti za vijana hao.
Licha ya askari wa Jeshi la Polisi kufika katika eneo la tukio hawakuweza kumkamata Katibu wa CCM wa wilaya na badala yake walimchukua Katibu wa Kata wa chama hicho, Waliadi Ngogo.

No comments:

Post a Comment